
Manchester, England. Michael Carrick amesema atajisikia yupo nyumbani akiwa Meneja Mkuu wa Manchester United baada lakini anaamini klabu hiyo haitafanya maamuzi ya haraka kama itampa nafasi hiyo au la.
Tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa Man United hadi mwisho wa msimu, Carrick ameiongoza kupata ushindi dhidi ya Manchester City, Arsenal na Fulham, jambo lililoifanya itinge nne bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL).
Carrick mwenye umri wa miaka 44 amekiri kuwa yupo kwenye orodha ya wanaoweza kupewa nafasi ya umeneja, lakini akasisitiza bado ni mapema kwa klabu kutoa uamuzi kwa kuzingatia matokeo machache tu.
“Naifurahia sana kazi ninayofanya. Nipo hapa na najisikia nyumbani, lakini ninaelewa kikamilifu hali ilivyo, hivyo sitaki kujipa matumaini kupita kiasi.
“Hakuna kilichobadilika. Kwa kweli, hilo halitabadilisha ninachokifanya au ninavyohisi. Ninafahamu vyema jukumu nililopewa na dhamana niliyonayo.
“Tunataka kufanikiwa. Nataka klabu ifanikiwe hata baada ya msimu huu kumalizika, iwe ni mimi au mtu mwingine. Kwa sasa siwezi kudhibiti hilo, tutasubiri tuone kitakachotokea,” alisema Carrick.
Kiungo huyo wa zamani wa Man United amesema kuwa jukumu lake kwa sasa ni kuhakikisha timu inakuwa na muendelezo mzuri.
“Jambo la msingi ni kuiboresha timu na kuendelea kuifanya Manchester United kuwa imara zaidi siku hadi siku. Hivyo matokeo ya muda mfupi hayapaswi kubadili hilo.
“Kama matokeo hayo yatafanya mabadiliko makubwa, basi kuna tatizo. Maamuzi hayawezi kuwa ya pupa iwe mambo yanaenda vizuri au kuna changamoto chache za kutatua. Kinachohitajika ni maendeleo ya taratibu.
“Soka linaweza kubadilika kwa haraka sana, hivyo ni lazima tubaki tulivu na kuzingatia kile tunachopaswa kufanya,” alisema Carrick.
Wasaidizi wa Carrick pia wamepata sifa kwa mchango wao katika mwanzo huo mzuri, baada ya kocha huyo kuwaleta aliyekuwa kocha msaidizi wa England na Chelsea, Steve Holland pamoja na msaidizi wake wa zamani wa Middlesbrough, Jonathan Woodgate, kufanya kazi na makocha wa Man United akiwemo Jonny Evans, Travis Binnion na Craig Mawson.
Carrick amefichua pia kuwa alizungumza na mdogo wake, Graeme, aliyefanya kazi katika Shirikisho la Soka England (FA) kwa miaka 15, kabla ya kuamua kumfuata Holland.
“Nilipoona mazungumzo yanaendelea na ikaonekana huenda nikaja hapa, nilitumia muda kufikiria muundo wa benchi la ufundi na kuzungumza na mdogo wangu, kama ninavyofanya mara kwa mara, kuhusu jinsi mambo yangekuwa,” aliongeza Carrick.