Manchester, England. Kocha wa muda wa Manchester United, Michael Carrick, amesema klabu hiyo haitafanya maamuzi ya haraka au ya pupa kuhusu mustakabali wake kama kocha mkuu, tofauti na ilivyofanya awali kwa Ole Gunnar Solskjaer.
Carrick aliteuliwa kuwa kocha wa muda hadi mwisho wa msimu mwezi uliopita na tayari ameonyesha mwanzo mzuri baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi katika mechi nne mfululizo.
Ushindi wa jana dhidi ya Tottenham Hotspur nyumbani uliifanya Manchester United kushinda mechi nne za Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu Februari 2024.
Mshambualiaji wa Man United, Bryan Mbeumo, (katikati) akishangilia bao lake katika ushindi wa 2-0 ilioupata Man United dhidi ya Spurs. Picha na Mtandao
Hata hivyo, Carrick anaelewa kuwa mafanikio ya muda mfupi hayataathiri mchakato wa klabu wa kumpata kocha mkuu wa kudumu.
Desemba 2018, Ole Gunnar Solskjaer aliteuliwa kuwa kocha wa muda na akaanza kwa msururu wa ushindi wa kushangaza wa mechi nane mfululizo.
Manchester United ilishinda mechi 14 kati ya 19 chini ya Solskjaer kabla ya kuthibitishwa rasmi kuwa kocha wa kudumu Machi 2019.
Lakini baada ya uteuzi huo, matokeo yalibadilika. United ilishinda mechi mbili pekee kati ya 10 za mwisho za msimu huo na kupoteza mara sita, hali iliyowagharimu nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa sasa, Mkurugenzi wa Soka wa Manchester United, Jason Wilcox, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu, Omar Berrada, wanaendelea na mchakato wa kumtafuta kocha mkuu wa kudumu kwa msimu ujao.
Kocha wa muda wa Man United, Michael Carrick, akizungumza jambo na kiungo wake, Kobbie Mainoo, baada ya mechi ya Ligi Kuu kati ya Man United na Spurs kumalizika Old Trafford. Picha na Mtandao
Carrick amesisitiza kuwa klabu haina mpango wa kubadili mwelekeo wake kabla msimu kumalizika Mei 24, akisema:
“Hakuna kilichobadilika. Kwa kweli, hilo halibadilishi ninachofanya wala ninavyojisikia. Ninafahamu nafasi yangu na wajibu wangu hapa. Tunachotaka ni kuona Manchester United inafanikiwa, iwe ni chini yangu au mtu mwingine baada ya msimu huu.”
Ameongeza kuwa lengo lake kuu kwa sasa ni kuiboresha timu na kuiweka katika msingi imara wa mafanikio ya muda mrefu.