
MATOKEO ya Yanga kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat yamewaumiza mashabiki na hata wachezaji wa timu hiyo, lakini kuna kauli ametoa kocha mkuu, Pedro Goncalves akisema safari yao imebakiza dakika 90 na hapo wataamua wenyewe waende robo fainali au watoke.
Yanga ilikumbana na kipigo hicho juzi usiku mjini Rabat, Morocco kwa kupoteza mbele ya wenyeji wao AS FAR Rabat matokeo ambayo yamewarudisha hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi tano, huku Wamorocco hao wakiruka nafasi ya pili wakifikisha pointi nane ambazo ni pungufu ya pointi moja ya zile anazozimiliki kinara wa kundi hilo Al Ahly yenye tisa.
Matokeo hayo yanaitaka Yanga kuhakikisha wanashinda nyumbani dhidi ya JS Kabylie ushindi wa tofauti ya mabao mawili na pia dua zao zikiwa Misri wakiiombea mabaya FAR Rabat ifungwe hata 1-0 itakayokuwa mgeni wa Ahly mechi zote zikipigwa Februari 15.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro amesema hayakuwa matokeo mazuri kwa timu hiyo na sasa wana kazi moja tu wao makocha na wachezaji wao kuhakikisha wanakwenda kuamua hatma yao dhidi ya JS Kabylie ili waende robo fainali au wasalie hapo.
Pedro amesema haikuwa rahisi kucheza vizuri sana kwa vijana wake kwenye mazingira ya hali ya hewa ya mvua kubwa, lakini wakafanya kosa moja kubwa ambalo lilikwenda kuamua mchezo huo huku akiwapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa umakini mkubwa kabla ya kuruhusu bao hilo.
“Ilikuwa mechi ngumu na ugumu ukaongezeka zaidi kutokana na aina ya hali ya hewa ambayo ilijitokeza katikati ya mchezo, ilikuwa ngumu kucheza kwenye mvua kubwa na baridi ndani yake lakini hata hivyo wachezaji wangu walipambana sana,” amesema Pedro ambaye amepoteza mchezo wa pili kwake tangu aanze kuifundisha timu hiyo,
“Tulifanya kosa moja la kujisahau ambalo liliamua mchezo, mimi sio muumini wa kukata tamaa hasa kwenye eneo ambalo bado tuna nafasi, tuna dakika 90 ngumu nyumbani ambazo tunatakiwa kwenda kuamua wenyewe kwenda robo fainali au tubaki.”
Pedro amesema kila timu ambayo imeshinda kwenye kundi hilo imetumia uwanja wa nyumbani ambapo nao Yanga wanatakiwa kufanya hivyo kwenye mchezo wa mwisho huku akiwataka mashabiki wao kuja kuwapa nguvu wachezaji wa timu hiyo.
“Kwangu mimi tunaweza kuvuka hapa nimewaambia wachezaji huu sio wakati wa kuendelea kuinamisha vichwa chini, tunatakiwa kubadilika haraka, timu zote ambazo zimeshinda kwenye kundi letu wameshinda nyumbani na sio ugenini,” amesema Pedro na kuongeza;
“Najua mashabiki wetu tumewaangusha lakini tunajua nguvu yao wakiwa na sisi pamoja, tutafanya marekebisho ya makosa yetu naamini ili tukirudi tuwe imara zaidi, nawaamini wachezaji wangu kwamba wataweza kucheza kwa hesabu kubwa.”
UJIO WA MZIZE
Aidha Pedro amesema kurejea kwa mshambuliaji wake Clement Mzize aliyepewa dakika 10 za mwisho kwenye mchezo wa juzi ni hatua kubwa ambapo itaongeza nguvu kuelekea mchezo huo wa mwisho wa makundi, utakaopigwa Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar.
“Kila mmoja ana furaha na kurejea kwa Clement (Mzize) ni mchezaji muhimu lakini angalia ndani ya dakika 10 alizocheza amejaribu kufanya kitu tofauti, ni mchezaji mwenye ari kubwa, naamini ataendelea kuimarika zaidi, tuliona tumpe dakika za mwisho ili tusije kufanya hatari kubwa kwake.”