Liverpool, England. Timu pekee zilizotwaa taji la Ligi Kuu England katika misimu minane iliyopita zitakutana wikendi hii na takwimu zinaonyesha kuwa mabingwa watetezi huenda wakatoka kifua mbele.
Tangu Chelsea ilipotwaa ubingwa msimu wa 2016–17, hakuna timu nyingine iliyoshinda taji hilo isipokuwa Liverpool au Manchester City, huku jeshi la Pep Guardiola likitwaa mataji sita na Liverpool mawili.
Lakini licha ya mafanikio yao, Uwanja wa Anfield umebaki kuwa kikwazo kikubwa ambacho Guardiola na Man City yake wamekuwa wakishindwa kukivuka. Kwa kweli, kocha huyo Mhispaniola ameshinda mara moja tu katika safari zake Anfield, ushindi wa 4-1 mnamo Februari 2021.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola (Kulia), aliewahikuwa mkurugenzi wa ufundi wa Man City, ambaye sasa ameondoka, Txiki Begiristain (Kushoto). Picha na Mtandao
Faraja ndogo kwa Man City ni kwamba ushindi huo ulipatikana wakati Liverpool walipokuwa mabingwa watetezi.
Lakini, hata kabla ya kuwasili kwa Guardiola, Man City ilikuwa ikipata tabu Anfield, huku ushindi huo wa miaka mitano iliyopita ukiwa pekee yao katika mechi zao 22 za mwisho uwanjani hapo.
Imepoteza mechi 14 na kutoka sare mara saba kati ya mechi 21 zilizopita, huku ushindi wao wa awali ukitokea Mei 2003, ambapo Nicolas Anelka alifunga mabao yote mawili, likiwemo bao la ushindi dakika za mwisho kufuta bao la Milan Baros. Huo ndio ushindi pekee mara mbili wa Man City kwenye Ligi Kuu England waliopata Anfield, kwani hata mshambuliaji wao nyota Erling Haaland amekuwa akipata ugumu hapo.
Anfield ni moja ya viwanja viwili tu vya Ligi Kuu England ambavyo mshambuliaji huyo wa Norway ameshindwa kufunga tangu ajiunge na Man City. Amecheza hapo mara tatu, na uwanja mwingine pekee aliokosa kufunga ni Stadium of Light, ambapo alicheza kwa mara ya kwanza msimu huu. Haaland amefunga bao moja tu la kimchezo katika mechi zake 12 za mwisho, bao hilo likitokea katika ushindi wa 2-0 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray mwezi uliopita.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola, (Kushoto), kulia ni kocha wa Liverpool, Arne Slot. Picha na Mtandao
Alifunga pia wakati Man City ilipoifunga Liverpool 3-0 mwezi Novemba na ushindi Anfield, Jumapili utawafanya wakamilishe ushindi wa pili dhidi ya mabingwa watetezi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 89 mara ya mwisho kufanya hivyo ikiwa ni msimu wa 1936/37, ambao pia ulikuwa mara ya mwisho kuwafunga Liverpool katika mechi mbili za ligi mfululizo.
Pia wanaweza kuwa timu ya kwanza kuifunga Liverpool bila kuruhusu bao mara mbili katika msimu mmoja tangu West Ham walipofanya hivyo msimu wa 2015–16. Mara nyingi husemwa kuwa bao la kwanza ni muhimu sana, lakini huenda isiwe hivyo katika mchezo huu.
Man City haijaruhusu bao lolote katika kipindi cha kwanza cha mechi za Ligi Kuu England mwaka 2026, wakifunga mabao sita, lakini rekodi yao kipindi cha pili ni tofauti kabisa, wakiruhusu mabao sita na kushindwa kufunga hata moja.