
Italia imesema haiwezi kujiunga na kinachoitwa “Bodi ya Amani” ya Rais wa Marekani Donald Trump kutokana na “mpaka wa kikatiba” ukiwa ni mkwamo mpya na wa karibuni zaidi kukikabili “chombo hicho cha kimataifa cha kujenga amani”, alichojibunia rais wa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani ametangaza kuwa, migongano iliyopo kati ya katiba ya Italia na hati ya ‘bodi ya amani, ya Trump “haiwezi kuvukwa kwa mtazamo wa kisheria”, hata hivyo, nchi yake itakuwa tayari “kujadili juhudi za amani” kuhusiana na Ghaza.
Italia inajiunga na nchi nyingine kadhaa za Ulaya waitifaki wa Marekani, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Ujerumani, na Uingereza, ambazo zimekataa kujiunga na bodi hiyo yenye utata, ambayo iliangaziwa na Umoja wa Mataifa mwaka jana kama chombo cha mpito cha utawala wa Ghaza baada ya vita, kabla ya kupanua wigo wake katika mkataba mkubwa ambao haukutaja eneo hilo la Wapalestina lililokumbwa na vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel.
Uamuzi huo wa Italia umetangazwa licha ya uhusiano wa karibu uliopo kati ya waziri mkuu wa nchi hiyo Giorgia Meloni na mwenyekiti wa bodi Trump huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kwamba bodi hiyo inayodaiwa kuwa mtatuzi wa migogoro duniani huenda ikawa inalenga kunyakua nafasi ya Umoja wa Mataifa.
Tajani ameashiria Kifungu cha 11 cha katiba ya Italia, ambacho kinazuia nchi hiyo kujiunga na mashirika isipokuwa kama kuna “masharti ya usawa kati yake na mataifa mengine”, hali ambayo haipo katika Hati ya bodi hiyo inayomtaja Trump kama mwenyekiti mwenye kura ya turufu anayehudumu kama mtu mwenye sauti ya mwisho.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia ametangaza msimamo huo huku bodi hiyo ya Trump inayoripotiwa kuwataka wanachama wake kulipa dola bilioni 1 kwa ajili ya kuwa na kiti cha kudumu, ikijiandaa kwa mkutano wake wa kwanza huko Washington, DC, mnamo Februari 19.
Mkutano huo utafanyika siku moja baada ya mkutano uliopangwa kati ya Trump na waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ambaye naye pia amejumuisha kwenye iitwayo bodi ya amani licha ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutoa waranti wa kumkamata kwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Ghaza.
Itakumbukwa kuwa mwezi uliopita, Trump alizialika karibu nchi 60 kujiunga na bodi hiyo.
Hii ni katika hali amabyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekosoa mpango huo wa Trump wa kuunda anachokiita bodi ya amani akisema “Jukumu la msingi la amani na usalama wa kimataifa liko mikononi mwa Umoja wa Mataifa, liko mikononi mwa Baraza la Usalama”…/