GEITA: KAMPUNI ya Madini ya Mwamba Mining imefadhili usafiri wa baiskeli 100 kwa wanafunzi wa shule mbili za sekondari wilayani Geita ili kuongeza mahudhurio ya vipindi shuleni na kuinua kiwango cha elimu.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi Sh milioni 80 umetolewa kwa ushirikiano na Shirika la Asante Africa Tanzania na kampuni ya Buffalo Bicycles walengwa wakiwa ni wanafunzi wanaoishi mbali na shule

Meneja wa Kampuni wa Mwamba Mining, Kelvin Habil ametoa taarifa hiyo wakati wa kukabidhi baiskeli iliyofanyika kata ya Lwamugasa na kutaja wanufaika ni shule za Sekondari Lwamugasa na Evarist.

Amesema hatua hiyo inakuja baada ya kubaini baadhi ya wanafunzi wanafeli masomo siyo kwa sababu hawana uwezo bali ni kwa kushindwa kuhudhuria vipindi kwa wakati na hata uchovu wa umbali mrefu.

Amesema hiyo ni awamu ya kwanza ya mpango wa kusaidia kuinua ufaulu wa wanafunzi shuleni unaotekelezwa na kampuni hiyo na utakelezaji utaendelea kwa awamu ili kuwafikia wanafunzi wengi.

“Baada ya hili tutaingia pia upande wa visima vya maji ili mtoto apate maji safi, kwani hata kama ana baiskeli akinywa maji machafu akaugua hata hiyo baiskeli hawezi kuiendesha’ amesema Habil.

Mkurugenzi wa Asante Africa Tanzania, Florence Thomas amesema kipaumbele kikubwa ni kwa watoto wa kike hasa kidato cha kwanza na cha pili kwani wengi ni wadogo kiumri na wanakutana na changamoto.

Mwakilishi wa kampuni ya Buffalo Bicycles, Bernardo Bulugu amesema baiskeli hizo zimezingatia ubora na mahitaji ya wanafunzi ambapo ugawaji utasimamiwa na kamati ya shule husika.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Yohana Katambi amekiri basikeli hizo zitaongeza mahudhuri na kupunguza tatizo la kukatisha masomo kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule.

Katibu Tawala a wilaya ya Geita, Lucy Beda amewataka wazazi kuchukua msaada huo kama nyenzo ya kuwainua watoto kielimu huku akisisitiza wale watakaobainika kuwapokonya watoto watachukuliwa hatua kali.

“Tunaomba sana wazazi tuwaachie watoto baiskeli hizi zifanye kazi iliyokusudiwa, tusione mzazi anampokonya mtoto baiskeli, kwani kufanya hivo ni kurudisha nyuma juhudi zinazofanyika,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *