Dodoma. Maduka ya kisasa 31 ya ‘Airtel Smart Shops’ yamezinduliwa nchini kote, ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha huduma kwa wateja na kuchochea upatikanaji wa huduma za kidigitali nchini.

Maduka haya mapya yaliyozinduliwa chini ya kaulimbiu ya ‘Airtel Kila Kona’, yana muundo wa kisasa na mifumo ya kidijitali inayounga mkono uhifadhi wa mazingira kupitia utendaji kazi usiotumia karatasi.

Wateja wanaweza kupata huduma kwa urahisi kupitia mifumo ya kidijitali, jambo linalohakikisha huduma ya haraka, rahisi, na salama.

Hafla rasmi ya uzinduzi imefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ambaye ameipongeza Airtel Tanzania kwa uwekezaji wake katika kuchochea ukuaji wa huduma za kidijitali nchini.

“Uzinduzi wa maduka haya ya kisasa nchi nzima umeonyesha dhamira ya Airtel katika kuunga mkono matumizi ya teknolojia, kuboresha utoaji wa huduma na kupanua ujumuishi wa kifedha. Ubunifu unaorahisisha upatikanaji wa mawasiliano na huduma za kifedha ni muhimu katika kuwawezesha wananchi na biashara, hasa wananchi wenye biashara ndogo na za kati, pamoja na kukuza uchumi wa kidijitali,” amesema Kairuki.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya Desemba 2025, umiliki wa simu janja nchini umefikia asilimia 41.8, ikiwa ni sawa na simu janja milioni 28.5 zinazotumika nchi nzima, hali inayoonyesha ukuaji wa haraka wa matumizi ya kidijitali.

Maduka ya Airtel yatakuwa muhimu katika kuchangia ukuaji wa eneo hilo kupitia suluhisho la mikopo ya simu janja kwa gharama nafuu na teknolojia ya 5G, huku zikisaidia zaidi ya biashara ndogo na za kati (SMEs) 12,000 zilizopo maeneo ya maduka hayo kupata intaneti ya kasi na huduma za kifedha za kidijitali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, alisema mpango huo ni sehemu ya  mkakati wa Airtel wa kupanua wigo wa  huduma bora na za uhakika kwa watanzania.

“Maduka haya yanakwenda kuleta mnageuzi katika utoaji wa huduma kwa wateja wetu. Pia, tunatengeneza mazingira ambapo watu binafsi na wananchi wenye biashara ndogo na za kati, takribani biashara 400 kwa kila duka, wanaweza kupata vifaa vya kidijitali, mawasiliano, na suluhisho za kifedha wanazohitaji ili kukua. Hii ni hatua kubwa kuelekea kukuza ujumuishi wa kidijitali, na kufungua fursa za kiuchumi,” amesema Bw. Kamoto.

Maeneo ya Maduka Mapya ya Smart Shops:Dodoma 4 Dar es Salaam12, Arusha 4, Mwanza 6, Zanzibar 4.

Aidha, upanuzi huu unatarajiwa kutengeneza fursa za ajira ikiwamo za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja hususan kupitia kuimarika kwa mtandao wa mawakala, jambo litakalochangia zaidi katika uwezeshaji wa kiuchumi na ajira kwa vijana.

Maduka haya yatakuwa vitovu vya kidijitali vinavyotoa huduma zote kwa pamoja (one-stop shop), yakitoa huduma za simu na intaneti, Airtel Money, na suluhisho la mikopo ya simu janja kwa zaidi ya wateja milioni 22.9.

Upanuzi wa Airtel Smart Shops nchi nzima unasisitiza dhamira ya Airtel Tanzania ya kuongoza mabadiliko ya kidijitali, kupanua ufikiaji wa huduma za kifedha, na kuwawezesha watu binafsi na biashara kote nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *