Florida, Marekani. Staa wa Inter Miami ya Marekani, Lionel Messi yupo katika mazungumzo na klabu yake ya utotoni, Newell’s Old Boys, ambayo imevutiwa zaidi baada ya staa huyo kuthibitisha ndoto yake ni kuichezea klabu hiyo tena.
Messi mwenye umri wa miaka 38 ni zao la akademi ya Newell’s ya Argentina, akiwahi kuitumikia kwa miaka saba katika timu za vijana kabla ya kujiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13.
Nyota huyo wa Argentina alifunga mabao 234 akiwa na timu za vijana za Newell’s, na katika Uwanja wa klabu hiyo kuna jukwaa ambalo limepewa jina lake.
Akizungumza na chombo cha habari cha Argentina, TN, makamu wa rais wa Newell’s, Juan Manuel Medina, amethibitisha kuwa mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya klabu hiyo kumsajili Messi hivi karibuni.
Nyota wa Inter Miami na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi akisalimiana na baadhi ya wachezaji wa Newell’s Old Boys. Picha na Mtandao
“Tunafanya kazi kuhakikisha Leo (Messi) anachezea Newell’s katika nusu ya kwanza ya mwaka 2027. Mpango wa kumleta hapa sio wetu pekee bali unahusisha Jiji la Rosario,na soka la Argentina kwa ujumla. Tunafahamu ili kumpata itahitaji kumshawishi juu ya mipango yetu.”
Kwa sasa, Messi bado ana mkataba na Inter Miami hadi mwaka 2028, baada ya kusaini mkataba mpya na klabu hiyo ya MLS Oktoba mwaka jana.
Hata hivyo, kwa kuwa msimu wa 2027 unatarajiwa kugawanywa ili ligi hiyo iendane na ratiba ya Ulaya, Messi anaweza kuangalia uwezekano wa kuhamia kwa mkopo wa muda mfupi Newell’s.
Picha ya kumbukukizi ikimuonyesha nyota wa Argentina, Lionel Messi (Katikati aliyeshika mpira) wakati alipokuwa akiitumikia timu yake ya utotoni, Newell’s Old Boys. Picha na Mtandao
Messi hajawahi kuficha mapenzi yake kwa klabu yake hiyo ya utotoni na mwaka 2017, alisema: “Nimesema mara nyingi kwamba ndoto yangu ni kuichezea Newell’s, lakini sijui nini kitatokea baadae, na kinachonipa mashaka kwa sasa ni hali ya kiusalama kudorora nchini kwangu. Nina familia na watoto. Wao ndio kipaumbele changu kwa sasa. Nataka wakue katika mazingira tulivu, wakifurahia maisha kwa usalama.”
Messi amecheza mechi 88 akiwa na Inter Miami tangu ajiunge na klabu hiyo, akifunga mabao 77. Pia ameisaidia kushinda MLS Cup, MLS Supporters’ Shield na Leagues Cup.