DAR ES SALAAM: Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, imesaini mikataba mitano itakayowawezesha vijana wa Kitanzania kupata ajira nje ya nchi, huku mikataba mingine 16 ikiwa katika hatua za mwisho za kukamilishwa ili kupanua zaidi fursa za ajira kwa vijana.

Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali katika kukuza uchumi na kufanikisha lengo la Taifa la kufikia pato la Dola Trilioni Moja za Kimarekani ifikapo mwaka 2050.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Februari 7, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wanapata ajira zenye tija ndani na nje ya nchi.

Waziri Sangu ameyasema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa kipindi cha Imbeju Bongo Fursa pamoja na jarida la Mapitio ya Vijana, ambavyo vinalenga kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo.

Aidha, Waziri Sangu ametumia jukwaa hilo kuiagiza CRDB Bank Foundation kuwazingatia vijana wabunifu waliopo chini ya Baraza la Taifa la Biashara na Maendeleo (NEDC), katika ufadhili wa shilingi bilioni 200 zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza bunifu za vijana.

Kwa upande wao, wakieleza umuhimu wa jarida na kipindi cha Imbeju Bongo Fursa katika kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi, Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Biashara na Maendeleo (NEDC), Bwana Jesse Madauda, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tullyesther Mwambapa, wamesema majukwaa hayo yataongeza uelewa wa vijana kuhusu fursa za kiuchumi na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *