Shambulio la ndege zisizo na rubani la Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF lililolenga gari lililobeba familia za raia wa Sudan waliolazimika kuyahama makazi yao limeua watu wasiopungua 24, wakiwemo watoto wanane. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la mtandao wa Madaktari wa Sudan.

Shirika hilo la Mtandao wa Madaktari wa Sudan, ambalo linafuatilia vita vinavyoendelea nchini humo limebainisha katika taarifa kwamba, shambulio hilo la jana Jumamosi lilitokea karibu na mji wa Rahad ulioko kwenye mkoa wa Kordofan Kaskazini katikati mwa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gari hilo lililoshambuliwa na kundi la RSF lilikuwa likisafirisha watu waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita huko eneo la Dubeiker Kordofan Kaskazini.

Mtandao wa madaktari wa Sudan umeongeza kuwa, miongoni mwa watoto waliouawa ni pamoja na watoto wachanga wawili.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Watoto UNICEF liliripoti siku ya Ijumaa kwamba, watoto wasiopungua 20 waliuawa mwezi Januari nchini Sudan, wengi wao katika maeneo ya Kordofan na Darfur magharibi mwa nchi.

Shirika hilo limetahadharisha kuwa “mamilioni ya watoto nchini Sudan wanahitaji misaada, ulinzi na kurejeshewa huduma za msingi” wakati mapigano yakiendelea kuharibu maeneo mengi ya nchi.

UNICEF imesema njaa kali tayari imethibitishwa Al Fasher Kaskazini mwa Darfur na Kadugli huko Kordofan, huku maeneo mengine karibu 20 yakiwa hatarini…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *