Dar es Salaam. Matokeo ya ushindi nyumbani leo dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria ndio ambayo yataiweka Singida Black Stars katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu tofauti na mengine.

Ikiwa inashika mkia katika kundi C la mashindano hayo na pointi zake nne, ikiibuka na ushindi katika mchezo wa leo uliopangwa kuanza saa 1:00 usiku, kutaifanya Singida Black Stars kufikisha pointi saba ambazo zinaweza kuisogeza hadi nafasi ya pili kutegemea matokeo ya mchezo baina ya AS Otoho na Stellenbosch.

Ikipata matokeo ya ushindi leo, maana yake itatakiwa kuibuka na ushindi katika mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Stellenbosch na kisha kuombea AS Otoho ili yenyewe itinge robo fainali.

Lakini kama itatoka sare leo, matumaini yake ya kufuzu robo fainali yanaweza kuzikwa rasmi leo ikiwa Otoho itapata ushindi wa nyumbani dhidi ya Stellenbosch kwani timu hiyo ya Congo itafikisha pointi tisa ambazo hazitoweza kufikiwa na Singida Black Stars.

Kwa Belouzdad, ushindi katika mechi ya leo sio tu utaifanya iwe na uhakika wa timeti ya robo fainali bali pia itajihakikishia uongozi rasmi wa kundi C.

Ni mechi ambayo inamrudisha Tanzania, kiungo Jean Charles Ahoua ambaye amejiunga na CR Belouzdad katika dirisha dogo la usajili mwaka huu akitokea Simba.

Mbali na Ahoua, mchezo huo pia unamrudisha nchini Kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic ambaye kwa sasa ndio Kocha Mkuu wa CR Belouizdad.

Zinakutana timu mbili ambazo safu zao za ulinzi zimekuwa na muendelezo wa kuruhusu nyavu zao kutikiswa ambapo Singida Black Stars katika mechi nne imefungwa mabao matano sawa na wastani wa bao 1.25 huku Belouizdad ikiwa imefungwa mabao manne sawa na wastani wa bao moja kwa mchezo.

Utofauti unaonekana upo katika safu zao za ushambuliaji ambapo Belouizdad imekuwa tishio zaidi ikifunga mabao manne sawa na wastani wa mabao mawili kwa mechi na Singida Black Stars imefunga mabao matatu sawa na wastani wa bao 0.75 kwa mechi.

Katika mchezo wa leo, Singida Black Stars itamkosa kipa wake Metacha Mnata kwa vile anatumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo uliopita dhidi ya AS Otoho ambao timu yake ilifungwa mabao 2-1.

Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Othmen Najjar alisema kuwa timu yake inajua umuhimu wa mchezo huo na itajitahidi kuhakikisha inapata ushindi.

“Tukiwa na pointi nne, nadhani hatima ipo mikononi mwetu. Ni mechi ngumu ya uhitaji dhidi ya vinara wa kundi lakini tunaamini katika nafasi yetu kuendelea kupambana na mwisho wa hatua hii ya makundi tufikie malengo yetu,” alisema Najjar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *