Tanzania, Uganda zafungua ukurasa mpya uchumiTanzania, Uganda zafungua ukurasa mpya uchumi

TANZANIA na Uganda zimefungua ukurasa mpya wa kiuchumi huku zikisisitiza haja ya kuondoa vikwazo vya kiuchumi vinavyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya kikanda.

Hayo ni miongoni mwa masuala manane yaliyozungumzwa na Rais Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwenye mazungumzo ya pamoja walipokutana Ikulu, Dar es Salaam jana wakati Museveni alipofanya ziara ya siku moja nchini.

Rais Samia alisema vikwazo vya kibiashara vya kikodi na visivyo vya kikodi vikiondolewa, biashara katika nchi za Afrika Mashariki itakua. Alisema biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imekua na kwamba wote wamekubaliana kuwa vikwazo vinavyowekwa na watendaji katika maeneo mbalimbali viondolewe, kutengeneza Soko la Afrika Mashariki.

“Na hili ndilo mzee alitumia muda mrefu kunieleza kuhusu Soko la Afrika Mashariki, tunazalisha, watu wa nje wanataka kutuletea vya kwao lakini sisi wenyewe tunazalisha na ziada lakini hatuna soko. Hilo nalo tumelizungumza kwa kiasi kikubwa,” alisema Rais Samia.

Alitaja mambo mengine waliyozungumza kuwa ni pamoja na mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga na kwamba kuanzia Julai 2026, huenda meli ya kwanza ya mafuta ikang’oa nanga kupeleka mafuta ghafi ughaibuni.

Alisema mazungumzo yao pia yamegusia mabomba mawili mengine kwa maana ya bomba la gesi linalotoa gesi Tanzania kupeleka nchini Uganda na bomba la mafuta safi kutoka Uganda kuja Tanzania kuelekea sokoni.

Sambamba na hayo, walizungumza pia suala la matumizi ya bandari za Tanzania kusafirisha mizigo ya Uganda kwa kutumia Reli ya Kisasa (SGR) kutoka bandari za Dar es Salaam na Tanga hadi Kanda ya Ziwa ambapo watatumia Ziwa Victoria kusafirisha mizigo hadi Uganda.

Kadhalika, Rais Samia alisema katika mazungumzo na mgeni wake walizungumzia namna Uganda itakavyounganisha SGR kutoka Lusahunga hadi Murongo nchini Uganda ili kuunganisha taifa hilo na bandari za Tanzania.

“Jambo lingine ni kuendelea kuzalisha nishati kwenye miradi ya ushirikiano itakayozalisha nishati kwa ajili ya matumizi yetu ndani ya nchi zetu mbili na kanda nzima kwa ujumla,” aliongeza Rais Samia.

Katika ushirikiano wa kimataifa, Rais Samia alimshukuru Rais Museveni kwa kukubali kumuondoa mgombea wa Uganda kiti cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambacho kinatakiwa mgombea kutoka Afrika Mashariki na kumpisha mgombea wa Tanzania.

“Vilevile Uganda nayo inagombania kiti kama hicho ndani ya Umoja wa Afrika nasi tumeahidi tunawapa nguvu ili waende wakafanikiwe katika hilo,” aliongeza.

Vilevile, Rais Samia alisema Tanzania itamuunga mkono Rais Museveni katika mkakati wake wa kuleta amani na mshikamano ndani ya nchi za Maziwa Makuu na kwamba itamuunga mkono atakavyotaka kufanikisha mkakati huo. Kwa upande wake, Rais Museveni alisema mafanikio yaliyopatikana kutokana na vita ya ukombozi, yaendane na mafanikio ya kiuchumi na uunganishaji wa masoko.

Alizitaka nchi za Afrika Mashariki kuhakikisha zinasonga mbele kiuchumi baada ya kufanikiwa kupata uhuru na kuwahimiza viongozi kuzidisha umakini ili kufanikisha ukombozi wa kiuchumi hususani katika uzalishaji mali.

“Baada ya uhuru tulipaswa kuwapatia watu wetu mambo makubwa mawili likiwemo kuwawezesha wananchi kuzalisha mali, bidhaa na huduma pamoja na kuuza katika masoko mbalimbali,” aliongeza Rais Museveni.

Aliongeza kuwa kuongeza na kupanua masoko ni lengo muhimu pia la ukombozi uliofanywa na viongozi wa kwanza mataifa ya Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa ujumla. Katika hatua nyingine, Rais Museveni alimshukuru Rais Samia kwa kuweka mipango mizuri ya kutengeneza vifaa vya treni ya kisasa na kuahidi kuwa Uganda itakuwa soko zuri la vifaa hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *