CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kinatarajia kuanzisha mtaala mpya wa masomo ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya (HSCM) kwa Wafamasia ili kuwawezesha wawe na ujuzi pamoja na uwezo mkubwa katika kusimamia bidhaa za afya.

Mratibu wa Mradi wa Senselet Tanzania, Profesa Eliangiringa Kaale kutoka Shule ya Ufamasia ya  Chuo Kikuu hicho amesema hayo katika  kikao kilichowakutanisha wadau wa Serikali, taasisi za udhibiti, vyuo vikuu, washirika wa maendeleo,na sekta binafsi  , mjini Morogoro.

Kikao hicho kilikuwa na lengo  kujadili, kuboresha na kuidhinisha mtaala mpya wa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya ambao utakaowapatia  ujuzi , uwezo na mifumo inayohitajika kwa wafamasia kuhusu Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi wa Bidhaa za Afya nchini Tanzania.

Profesa Kaale amesema kuandaliwa kwa mtaala huo ni zao la  sherehe ya miaka 50 ya Shule ya Ufamasia (School of Pharmacy) ya Chuo Kikuu  hicho tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1974 ambayo  ilifanyika Novemba  2024.

Amesema  katika mawazo na maboresho ambayo wadau waliyaotoa kwa chuo hicho  wakati huo ni pamoja na kuboresha au kutoa ujuzi kwa wafamasia ili waweze kusimamia mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.

Profesa Kaale amesema wadau wa Chuo hicho walisisitiza  zaidi na Shule hiyo  kupitia uongozi wake uliweza  kuwafikia wadau wake wa maendeleo kwa maana ya Shirika la Kuhne Foundation lenye makao yake  nchini Ujerumani pamoja na Taasisi ya NOVO Nordisk ya Denmarkna kuwauzia hilo wazo.

“ Wadau hawa waliona wazo hili ni  zuri na walionesha nia ya kutufadhili na kwa sasa wametupatia  fedha kwa ajili ya kutengeneza mtaala ambao utawaandaa wafamasia waweze kumudu vyema masomo yao shahada katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya,”amesema  Profesa Kaale.

Profesa Kaale amesema  kwa sasa wanategemea baada ya kutekeleza mtaala huo wafamasia ambao watahitimu ngazi ya shahada kutoka Shule ya Ufamasia watakuwa wanaujuzi katika kusimamia bidhaa za afya kwa ujumla wake kwa maana ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kuhne Foudation Tanzania, Dk Beatrice  Millu alisema Shirika hilo limeanza kufanya kazi mwaka 2012 hapa nchini kwa mashirikiano na Vyuo Vikuu mbalimbali nchini ikiwemo MUHAS.

Dk Beatrice amesema  Shirika hilo linaamini uchumi katika Taifa lolote lile Duniani unategemea ukuaji bora wa usafirishaji, uchukuzi na ugavi wa bidhaa za afya  na kupitia mradi wa Senselet Tanzania wamekisaidia  Chuo Kikuu hicho katika jitihada zake kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ya usafirishaji ,uchukuzi  na ugavi katika mnyororo wa  bidhaa za afya .

“ Masuala ya afya kumeonenaka yana changamoto mbalimbali ambazo inahusisha kwenye usafirishaji ,uchukuzi , manunuzi na mengine yanaayoendana na sekta ya afya” amesema Dk Beatrice .

Dk Beatrice amesema , Shirika kwa kushirikiana na wadau wengine wamewezesha msaada wa kuona ni kwa jinsi gani jamii inaweza kupata huduma za afya zilizosalama na zenye usahihi zaidi kuanzia  masuala ya manunuzi , usafirishaji ,ufugaishaji na bidhaa inapomfikia mtumiaji wa mwisho ikiwa na ubora  unatarajiwa uliotokea nao kiwandani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *