Tabora. Zaidi ya wananchi 300,000 katika wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama yanayotoka Ziwa Victoria kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika wilaya za Sikonge, Urambo na Kaliua.
Akizungumza Februari 7, 2026 baada ya kuzindua mradi huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema utekelezaji wa mradi katika wilaya ya Sikonge umekamilika na wananchi wameanza kupata maji, huku akisema kuwa miradi ya Urambo na Kaliua inatarajiwa kukamilika ndani ya wiki tatu zijazo.
Aweso amemuagiza mkandarasi kuhakikisha mita 600 zilizobaki za ulazaji wa mabomba na usambazaji wa mtandao wa maji zinakamilika ndani ya muda huo ili wananchi waanze kunufaika mara moja.
“Mita 600 ni chache sana. Fanyeni kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Wameteseka kwa muda mrefu, hatutaki kuona wanaendelea kuteseka,” amesema.
Aidha, ameonya watendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) wanaohusika na usomaji wa mita kuacha mara moja tabia ya kubambikizia wananchi bili zisizoendana na matumizi halisi ya maji.
“Sitaki kusikia malalamiko ya bili zinazozidi matumizi. Mtu alipe kwa uniti alizotumia. Mtendaji yeyote atakayezingua, tutazinguana na habari itaishia hapo,” ameagiza.
Wananchi wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati akizungumza katika ziara yake mkoani hapo.
Mbunge wa Jimbo la Sikonge, Amosi Maganga, amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi kwani muda uliokuwa ukipotea kutafuta maji sasa utatumika kwenye shughuli za uzalishaji.
Mkazi wa Sikonge, Amina Juma, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukamilika kwa mradi huo akisema awali walikuwa wanalazimika kununua dumu moja la maji kwa Sh1,000 au kutumia maji ya visima ambavyo si salama.
“Tumepitia magumu sana. Uchumi wetu ni mdogo lakini dumu la maji lilikuwa Sh1,000. Sasa maji yamepatikana, tunashukuru sana,” amesema.
Wakati huo huo, akiwa wilayani Urambo kukagua mradi kama huo, Aweso ametoa Sh500 milioni kwa ajili ya usambazaji wa mtandao wa mabomba kwa wananchi ili maji yaanze kufika majumbani mara baada ya kukamilika kwa mradi, pamoja na Sh400 milioni kwa ajili ya umaliziaji wa bwawa la Kalemela.
“Nataka kazi zote ziende sambamba ili kila kitu kikamilike ndani ya wiki tatu,” amesisitiza.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA mkoa wa Tabora, Mayunga Kashilimu, amesema zimesalia mita 600 tu kufikisha maji katika tanki la Urambo na kwamba kazi inaendelea vizuri.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magret Sitta, amemshukuru waziri kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kuomba ukamilike ndani ya muda uliopangwa kutokana na changamoto kubwa ya maji inayowakabili wananchi.
“Wananchi wa Urambo wanateseka sana na ukosefu wa maji safi na salama. Hata utulivu majumbani hakuna. Tunahitaji maji ya uhakika,” amesema.