Zanzibar. Nguli wa muziki kutoka Mali, Salif Keita ameshindwa kupanda kwenye jukwaa la Sauti za Busara 2026, kutokana na matatizo ya kiafya. Nyota huyo alitarajiwa kuwa msanii atakayefunga tamasha hilo Februari 8,2026 lakini mambo yamekuwa tofauti.
Licha ya kushindwa kufika kwenye tamasha hilo ametuma watoto wake kumuwakilisha kwa kutumbuiza nyimbo zake. Akizungumza kuhusiana na kutofika kwa msanii huyo Mkurugenzi wa tamasha hilo Journey Ramadhan amesema licha ya changamoto iliyojitokeza tamasha limeisha vizuri
“Nawashukuru wote tuliokuwa pamoja tangu mwanzo. Pamoja na hayo tulikuwa na mzee wetu ambaye tulikuwa tunatarajia kuwa nae wa kutufungia tamasha, ambaye tumemtangaza tangu mwezi wa kumi. Lakini kwa bahati mbaya sana tulipata taarifa zake za ugonjwa ambapo yeye mwenyewe alikuwa hataki kukosa tamasha kwa sababu alisubiri kwa muda mrefu.
“Taarifa yake rasmi kutoka kwa dokta wake imelazimu yeye kutoweza kushirikiana nasi. Kwahiyo pamoja na hayo tulikuwa na majadiliano tukasema bora tubadilishe lineup kwa kumbadilisha headliner lakini ni utaratibu mgumu sana,”amesema
Amesema baada ya kufanya majadiliano na nguli huyo muafaka ulikuwa vijana wake kumuwakilisha.
“Tukafanya majadiliano na muhusika kanasema anadhani kuna vijana wake. Wale mliowaona na kile walichofanya ni yeye amewapa husia kwamba hata kama atatoweka duniani wale waendelee na amewapa ruhusa kuendelea na nyimbo zake.
“Ndiyo maana mmeona nyimbo zimeendelea vizuri lakini kwetu sisi siyo jambo baya ni zuri. Kwasababu kutokuwepo kwa Salif Keita siyo mwisho lengo ni kuwapa watu nafasi. Kaulimbiu yetu ni ‘Let Then Shine’ lengo ni kuwapa nafasi wanawake na watoto pale tumeona bendi imefanya kazi yake,”amesema
Aidha Journey amefunga tamasha hilo na kueleza kuwa kwa mwaka 2027 ambapo litakuwa msimu wa 24 litafanyika March na siyo Februari kama ambavyo hufanyika.
“Kwa mwaka 2027 tamasha litafanyika mwezi wa tatu tutapisha, Ramadhan lakini tutapisha pia kadhia ya mvua isije kutukuta,”amesema
Licha ya hayo kutokana na kushindwa kufika kwa msanii huyo, katika viwanja vya Manazi Mmoja ambapo linafanyika tamasha hilo ilioneshwa video ya Salif akielezea masikitiko yake.
“Mabibi, mabinti na mabwana, mashabiki wangu wapendwa wa Zanzibar na Tanzania, pamoja na wateja wote watakaokuja kwa ajili ya tamasha la Salif Keita. Naomba radhi. Naomba radhi sana, samahani. Nawajulisha kuwa mnisamehe kwa sababu ya tatizo la afya, sitaweza kufika Zanzibar.
“Lakini watoto wangu watakuja. Watoto hao wanafahamu kila kitu kuhusu Salif Keita. Wao ni kama Salif Keita mwenyewe. Watawaletea burudani. Mimi nitakuja Zanzibar wakati mwingine, kwa sababu ni nchi ninayoipenda. Ni nchi ambayo imekuwa ikionyesha uaminifu wake kwa utamaduni wa Afrika, na ni mahali pa utalii ningependa sana kutembelea na kuunga mkono. Asanteni sana na mpaka wakati mwingine,”alisikika Salif Keita