Katika hatua inayolenga kuhakikisha miradi mikubwa inafanikiwa, huku sekta binafsi ikipata usaidizi wa kiufundi na kifedha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshauriwa kufungua milango ya uwekezaji katika mafunzo, teknolojia, na mitaji kwa wazawa ili kuimarisha uwezo wao katika sekta ya ujenzi.

Ikiwa mstari wa mbele katika jitihada hizi, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), kwa kushirikiana na serikali katika uwezeshaji wa miradi mikubwa, imeibuka mshindi wa tuzo ya Benki Bora katika Kuwezesha Miradi ya Ujenzi Zanzibar kwenye Tuzo za Kimataifa za Ujenzi Zanzibar (ZICA Awards) zilizofanyika mwishoni mwa wiki Zanzibar.

Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Uwekezaji wa NBC, Elvis Ndunguru, amesema benki itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wa sekta binafsi katika miradi kama ujenzi wa Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi na Kituo cha Afya cha Kizimkazi. “NBC imeendelea kuwa mstari wa mbele katika miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo miradi ya reli, madaraja, na viwanja vya ndege. Sekta ya ujenzi ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi, hivyo tutaendelea kushirikiana na serikali na sekta binafsi kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa,” amesema Ndunguru.

Mwenyekiti wa Chama cha Taifa cha Biashara Zanzibar (ZNCC), Ali Suleiman Amour, ameeleza kuwa tuzo za ZICA ni jukwaa muhimu la kuhamasisha ubora, uwajibikaji, na ushindani wa kitaaluma katika sekta ya ujenzi. Pia aliwasihi serikali na wadau wa sekta binafsi kuendeleza ushirikiano, kukuza uwekezaji, na kuimarisha imani kati ya jamii na wajasiriamali.

#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *