Habari kubwa juzi nchini England ni ile ya mwanamuziki nyota wa Pop kuonekana katika viwanja vya soka akifuatilia mechi za mpira wa miguu kwa vijana wa kike wenye umri mdogo.

Madonna amewahi kujitambulisha kama “Mama wa Soka” kutokana na hamasa yake ya kuwashangilia mabinti zake katika changamoto na safari ya soka la vijana.

Safari hiyo sasa imepanda ngazi nyingine baada ya Malkia wa Pop kuwaunga mkono mapacha wake wenye umri wa miaka 13, Stella na Estere, walipokuwa wakicheza mechi ya kituo cha soka cha Tottenham chini ya umri wa miaka 14, Jumamosi.

Akiweka picha za mabinti hao wakicheza soka jijini London, Madonna ameandika kwenye Instagram: “Nitamwomba MUNGU kwa ajili ya jua kidogo!”

Katika ujumbe mwingine, nyota huyo wa muziki mwenye umri wa miaka 67 aliongeza: “Hongereni Stella na Estere, Hotspurs wameshinda!!! 5-0.”

Baada ya hapo, Madonna alisafiri kwa kile alichokiita “Uber yake ya pili tu kuwahi kupanda” kuelekea Uwanja wa Tottenham Hotspur Jumapili, kushuhudia mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake (WSL) kati ya Tottenham na Chelsea.

Alionekana akiwa jukwaani kaskazini mwa London, akijisitiri kwa miwani ya jua, akiwa pamoja na mpenzi wake mwenye umri wa miaka 29, Akeem Morris, pamoja na mabinti zake waliovaa mavazi ya Spurs.

Si mara ya kwanza kwa Madonna kuhudhuria mechi za soka London. Oktoba mwaka jana alionekana Stamford Bridge akiwa na Morris, wakishuhudia Chelsea ikiikaribisha Liverpool.

Morris, raia wa Jamaica, naye ni mpenzi wa soka ingawa hakuwahi kujijengea taaluma ya kulipwa. Aliwahi kucheza katika timu kadhaa za Marekani, ikiwemo NY Renegades FC.

Madonna pia huendelea kuonyesha mara kwa mara picha zake katika viwanja vya soka nchini Marekani kupitia mitandao ya kijamii, ambako mapacha wake wamekuwa wakicheza kwa kiasi kikubwa.

Novemba 2024, alituma mkusanyiko wa picha zilizowaonyesha Stella na Estere, akiandika: “Maisha ya Mama wa Soka. Msinipe pasi na kinywaji kwa wakati mmoja!

Madonna pia aliwahi kuhamishia maisha yake Lisbon mwaka 2017 ili kumuunga mkono mwanawe David Banda kufuata ndoto ya soka. David aliingia akademi ya Benfica akiwa na umri wa miaka 12, lakini hakufanikiwa kucheza soka la kulipwa na sasa anajishughulisha na utunzi wa muziki.

Inaaminika Madonna alianza kuhudhuria mechi za soka nchini Uingereza alipokuwa ameolewa na muongozaji wa filamu Guy Ritchie, shabiki mkubwa wa Chelsea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *