
Rais Masoud Pezeshkian amepongeza duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani na kuitaja kuwa “hatua ya kusonga mbele,” akisisitiza kuwa msimamo wa Tehran kuhusu suala hilo unategemea haki zilizoainishwa ndani ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Katika ujumbe aliouchapisha Jumapili kwenye jukwaa la mitandao ya kijamii X, Pezeshkian alisema: “Mazungumzo ya Iran na Marekani, yaliyofanyika kufuatia maombi ya serikali rafiki katika eneo hili, yalikuwa hatua moja mbele. Mazungumzo daima yamekuwa mkakati wetu wa kupata suluhu ya amani. Mantiki yetu kuhusu suala la nyuklia inajikita katika haki zilizoainishwa ndani ya NPT.”
Aliongeza kuwa taifa la Iran limekuwa likijibu lugha ya heshima kwa heshima sawia, lakini kamwe halivumilii lugha ya nguvu na vitisho.
Duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani, yakiratibiwa na Oman, ilikamilika Ijumaa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Muscat, baada ya saa kadhaa za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja. Majadiliano hayo, yaliyoanza asubuhi, yaliwezeshwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr bin Hamad Al Busaidi.
Ujumbe wa majadiliano kutoka Iran na Marekani ulibadilishana mitazamo, hoja na mbinu mbalimbali kupitia kwa mwanadiplomasia mkuu wa Oman.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ameeleza mazungumzo hayo kwa ujumla kuwa ni mwanzo mzuri, akisema misimamo ya Iran iliwasilishwa kwa uwazi na hoja zake zikafikishwa kwa wajumbe wa Marekani.
Katika uwanja wa nyuklia, Iran inasisitiza haki yake ya kisheria ya kurutubisha urani ndani ya ardhi yake, ikilitaja suala hilo kuwa mstari mwekundu katika mazungumzo.
Kwa mtazamo wa Tehran, hatua zozote za kiufundi zinaweza tu kuzingatiwa ndani ya mfumo unaotambua haki hiyo; masharti yoyote yanayozidi hapo yatachukuliwa kama ishara ya kukosa nia njema kutoka upande wa pili.
Iran ilikuwa imefanya duru tano za mazungumzo kuhusu mbadala wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, kabla ya mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel dhidi ya nchi hii na miundombinu yake ya nyuklia katikati ya mwezi Juni mwaka jana.