
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Akili Alumni Marathon 2026, tukio la kipekee litakalowaunganisha Watanzania waliowahi kusoma vyuo vikuu nje ya nchi ili kukimbia kwa lengo la kuwekeza katika kizazi kijacho.
Mkurugenzi wa Akili Education, Felician Chizelema, amesema marathon hiyo inalenga kukusanya USD 1.2 milioni zitakazotumika kufadhili wanafunzi 100 kusoma kozi za kisasa zenye mahitaji makubwa duniani, ambazo ni Artificial Intelligence, Cyber Security, na Blockchain Technology.
Amesema kuwa kila USD 12,000 itakayokusanywa itagharamia mwanafunzi mmoja kwa kipindi cha miaka minne, ikijumuisha ada, malazi, chakula, pamoja na gharama muhimu za safari.
“Lengo ni kuwapa vijana wa Kitanzania elimu ya teknolojia ya kiwango cha kimataifa ili warudi na kuchangia maendeleo ya taifa na tunazongatia zaidi wanafunzi ambayo hawajiwezi na wanandoto ya kusoma nje ya Tanzania,”
Chizelema amesema Akili Alumni Marathon itafanyika Aprili 6 2026, siku ya Jumatatu ya Pasaka, jijini Dar es Salaam, ikiwa na kaulimbiu ‘Run the Future’ 100 Scholarships for Tech Leaders.
“Tukio hilo linatarajiwa kuwakutanisha maelfu ya wahitimu, makampuni, taasisi, na wadau wa maendeleo kwa lengo la pamoja la kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa teknolojia,” amesema na kuongeza;
“Kupitia jukwaa hili, wahitimu wote waliowahi kusoma nje ya nchi wanahimizwa kushiriki, kukimbia, na kuchangia ili kusaidia kufanikisha ufadhili wa wanafunzi 100 na kuimarisha mustakabali wa taifa.”