Akilihutubia Baraza mjini Geneva baada ya ziara yake nchini Sudan, Türk amesema maelfu ya raia waliuawa ndani ya siku chache tu mwezi Oktoba mwaka jana, baada ya miezi 18 ya mashambulizi na kunyimwa mahitaji ya msingi. 

“Wajibu wetu wa pamoja ni kuwawajibisha waliohusika, na kuhakikisha hili halitokei tena,” amesema.

Manusura wasimulia mauaji ya halaiki na ya kiholela

Türk amesema ushuhuda uliokusanywa na ofisi yake unaonesha taswira ya kutisha ya uhalifu mkubwa uliotekelezwa wakati wa mashambulizi ya mwisho ya RSF. Wafanyakazi wake waliwahoji zaidi ya waathirika na mashahidi 140 nchini Sudan na mashariki mwa Chad, ambao wameripoti kwa uthabiti mauaji ya halaiki, mauaji ya kiholela na mashambulizi dhidi ya raia walipokuwa wakikimbia mji.

“Mara chache nimewaona watu wakiwa na mshtuko mkubwa kiasi hiki kutokana na waliyoipitia,” Türk amesema, akiongeza kuwa manusura wameelezea kuona miili ya watu ikiwa imetapakaa barabarani wakikimbia El Fasher, katika mandhari ambayo “mtu mmoja aliifananisha na siku ya hukumu.”

Kulengwa kwa misingi ya kikabila 

Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu, mashahidi wametoa simulizi zinazofanana kuhusu mauaji ya halaiki ya mamia ya watu waliokuwa wamejisitiri katika Chuo Kikuu cha El Fasher, pamoja na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na wahudumu wa afya. Türk amesema Ofisi yake ilipokea ushahidi wa kuaminika kwamba baadhi ya waathirika walilengwa kwa misingi ya kikabila, hususan watu wa kabila la Zaghawa. 

“Watu waliokimbilia maeneo tofauti, yaliyotengana kwa maelfu ya kilomita, walitoa maelezo yanayofanana kwa namna ya kushangaza,” amesema, akisisitiza ukubwa na uratibu wa mashambulizi hayo.

Kikundi cha watoto waliohamishwa na familia zao wamekaa pamoja katika kituo cha kukaribisha huko Tawila, Darfur Kaskazini, Sudan, baada ya kukimbia vurugu huko Al Fasher.

© UNICEF/Mohammed Jamal

Familia iliyofurushwa na vita imeketi pamoja katika kituo cha mapokezi huko Tawila, Darfur Kaskazini, baada ya kukimbia vurugu huko Al Fasher.

Ukatili wa kijinsia watumika kama silaha ya vita

Türk amesema unyanyasaji wa kijinsia umetumika “kwa utaratibu kama silaha ya vita” na RSF na wanamgambo waliokuwa washirika wao. 

Wakati wa ziara yake Sudan, Türk alikutana na manusura waliotoa ushuhuda wa ubakaji wa makundi na aina nyingine za ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana. 

Ofisi yake pia imerekodi visa vya ukatili wakati wa utekaji nyara na upekuzi wa wanawake na wasichana waliokuwa wakijaribu kukimbia. 

“Ushuhuda ulikuwa thabiti, wa kutisha na wa kuhuzunisha sana,” amesema.

Utekaji nyara, mateso na kusajili watoto vitani

Taarifa hiyo pia imeeleza kuhusu utekaji nyara wa raia kwa ajili ya fidia, kutoweka kwa watu kwa nguvu na hali zisizo za kibinadamu katika maeneo ya kizuizini. Maelfu ya watu bado hawajulikani walipo, Türk amesema, huku wengi wakiaminika kuhamishiwa katika gereza la Tagris mjini Nyala, Darfur Kusini. Wafungwa wa zamani waliripoti kuwa zaidi ya wanaume 2,000 walizuiliwa katika Hospitali ya Watoto ya El Fasher, na kwamba waliokufa walipelekwa kuzikwa karibu na hospitali hiyo. 

Türk pia amethibitisha kuwa ofisi yake imebaini kusajiliwa na kutumiwa kwa watoto na kundi la RSF, ama kwa kulazimishwa au kwa kuwekwa chini ya shinikizo la kijamii.

Hatari ya kurudiwa kwa ukatili

Türk amesema ofisi yake ilikuwa imetoa tahadhari kwa zaidi ya mwaka mmoja kuhusu hatari ya uhalifu wa mauaji ya halaiki huko El Fasher, lakini maonyo hayo hayakuzingatiwa. 

“Hatari ilikuwa wazi, lakini maonyo yetu yalipuuzwa,” ameliambia Baraza la Haki za Binadamu, akiweka jukumu la uhalifu huo moja kwa moja kwa RSF na washirika wao. 

Ameonya kuwa ukiukwaji kama huo unaweza kujirudia katika eneo la Kordofan, na akaitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka. 

“Iwapo tutakaa kando tukishika vichwa vyetu huku majeshi na makundi yenye silaha yakitekeleza uhalifu wa kimataifa uliotangazwa wazi,” amesema, “tunaweza kutarajia yajayo yaliyo mabaya zaidi .”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *