
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM leo Februari 9, 2026, kupitia taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na Tripoli Libya, limesema kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba watu 55, lakini wanawake wawili pekee raia wa Nigeria ndio wamepatikana wakiwa hai ambapo mmoja ameripoti kumpoteza mumewe, huku mwingine akisema amewapoteza watoto wake wawili wachanga katika ajali hiyo.
Msemaji wa IOM amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema kuwa timu za IOM zimefanya kazi ya ziada kutoa msaada wa matibabu kwa manusura hao mara tu walipofikishwa nchi kavu.
Kulingana na maelezo ya walionusurika, boti hiyo iliyokuwa imejaa watu kupindukia kutoka nchi mbalimbali za Afrika iliondoka eneo la Al-Zawiya nchini Libya majira ya saa tano usiku mnamo Februari 5 mwaka 2026, lakini baada ya mwendo wa saa sita, maji yalianza kuingia ndani na kusababisha ipinduke.
Wasafirishaji haramu wa binadamu watumia shida za watu kuwalaghai
Shirika hilo limeonya kuwa makundi ya wasafarishaji haramu wa binadamu yanaendelea kutumia vibaya shida za watu kwa kuwapandisha kwenye boti mbovu ambazo hazina uwezo wa kuhimili mawimbi makubwa ya baharini.
Hii sio boti ya kwanza kuzama kwenye njia hii
Takwimu za IOM zimeonesha kuwa mwezi Januari pekee, takriban watu 375 wamekufa au kupotea kwenye njia hii hatari ya kwenda Ulaya kupitia katikati ya bahari ya Mediterania kutokana na hali mbaya ya hewa.
Shirika la IOM linaomboleza vifo vya watu katika ajali nyingine kwenye njia hii ya Mediterania. Matukio haya yanayojirudia yanathibitisha hatari kubwa na za kifo wanazokumbana nazo wahamiaji na wakimbizi wanaojaribu safari hizi za hatari.
“Msiba huu ni kumbusho lingine kwa dunia kuwa safari za baharini kuelekea Ulaya kwa kutumia njia zisizo rasmi ni mlango wa kifo,” imesema IOM.
Waliokufa tangu Januari hadi sasa ni watu 484
Hali imekuwa mbaya zaidi, kwani tangu mwanzoni mwa mwaka 2025, zaidi ya watu 1,300 wamepotea baharini, na ajali hii ya sasa imefanya idadi ya watu waliofariki mwaka huu wa 2026 kufikia takribani watu 484.
Kupitia mradi wake wa Wahamiaji Waliopotea, IOM imebainisha kuwa vifo vingi havirekodiwi kabisa huku ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano imara wa kimataifa na hatua zinazojali ulinzi wa binadamu ili kukabiliana na mitandao ya walanguzi, pamoja na kuwepo kwa njia salama na rasmi za uhamiaji ili kupunguza hatari na kuokoa maisha.