
Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya kina mama na mtoto katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, lakini nyuma ya mafanikio hayo bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto na afya ya mtoto.
Wakati Taifa likiendelea na jitihada za kuokoa maisha ya watoto wachanga na walio na umri chini ya miaka mitano, ukosefu wa wataalamu waliobobea umeibuka kuwa mojawapo ya tishio kubwa linaloweza kuhatarisha uendelevu na kasi ya mafanikio yaliyopatikana.
Ni pengo hilo ambalo Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) sasa kinasaidia kuliziba, kufuatia kuhitimu kwa kundi la kwanza la wataalamu wa ndani waliopata mafunzo ya uzamili katika magonjwa ya watoto na afya ya mtoto kupitia mpango wake wa ‘Postgraduate Medical Education’
Kutokana na hali hiyo, afya ya mtoto bado ni miongoni mwa changamoto kubwa zaidi za sekta ya afya Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti za kitaifa na kimataifa za afya, vifo vya watoto wachanga yaani vifo vinavyotokea ndani ya siku 28 za mwanzo wa maisha vinachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Wakati vifo vya kina mama vimepungua kwa kasi katika miaka ya karibuni, vifo vya watoto wachanga na watoto wadogo vinapungua kwa mwendo wa taratibu zaidi, jambo linaloashiria kuwepo kwa matatizo ya kina katika mfumo wa huduma za afya, ikiwemo upungufu wa ujuzi na uhaba wa wataalamu bingwa.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha mara kwa mara kuwa Tanzania ipo mbali na viwango vinavyopendekezwa vya uwepo wa madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto.
WHO inapendekeza kuwa daktari mmoja wa watoto asihudumie zaidi ya watoto 50 wenye mahitaji tata ya kiafya. Hata hivyo, hali halisi Tanzania ni tofauti kabisa, ambapo katika maeneo mengi daktari mmoja wa watoto huhudumia zaidi ya watoto 10,000.
“Pengo hili linaeleza kwa nini bado tunashuhudia vifo vinavyoweza kuzuilika,” amesema Profesa Pascal Ruggajo ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Udaktari cha Aga Khan.
Profesa Ruggajo ameongeza; “Kama Taifa, tumepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya kina mama. Sasa mwelekeo wa kitaifa unaelekezwa kwenye uhai wa watoto, hususan watoto wachanga walio chini ya siku 28.
“Ili kufanikisha hili, lazima tuwe na wataalamu waliopata mafunzo maalumu ya kukabiliana na magonjwa na changamoto tata za utotoni.”
Hilo limezungumziwa pia na mmoja wa wahitimu wapya wa shahada ya uzamili ya magonjwa ya watoto na afya ya mtoto kutoka AKU, Dk Elisamia Ngowi, amesema uhaba wa wataalamu bado ni mkubwa na unaotia wasiwasi.
“Tupo nyuma sana katika idadi ya madaktari bingwa wa watoto. Uwiano tulio nao sasa hauwezi kuhimili mahitaji. Daktari mmoja hawezi kuwahudumia ipasavyo maelfu ya watoto,” amesema.
Ameongoza kuwa mafunzo ya ubingwa yanawapa madaktari uwezo wa kutambua changamoto kubwa za kiafya kwa haraka, hata katika mazingira yenye rasilimali chache.
“Kwa ujuzi tulioupata, tunaweza kugundua matatizo muhimu mapema na kuyasimamia kwa ufanisi zaidi. Pia tutawafundisha na kuwashauri madaktari wengine, hivyo kujenga uwezo huku taifa likiendelea kuongeza idadi ya wataalamu,” amesema Dk Ngowi.
Akifafanua wakati wa mahafali ya AKU ya mwaka 2026 yaliyofanyika leo Februari 10, 2026 jijini Dar es Salaam, Profesa Ruggajo amesema kuhitimu kwa kundi la kwanza la madaktari bingwa wa watoto ni hatua muhimu katika kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya afya nchini.
“Kwa kuzalisha wataalamu hawa, AKU inachangia moja kwa moja mapambano ya kitaifa dhidi ya vifo vya watoto. Tunaongeza nguvu kazi yenye ujuzi mstari wa mbele,” amesema.
Mahafali hayo yamefanyika wakati Serikali ikiendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya. Upanuzi wa miundombinu ya afya, kuboreshwa kwa vituo vya kutolea huduma na kuajiriwa kwa wahudumu zaidi wa afya kumechangia kwa kiasi kikubwa kuboreshwa kwa matokeo ya afya ya kina mama.
Juhudi hizo zilitambuliwa kimataifa mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alipotunukiwa Tuzo ya Goalkeepers kutoka Taasisi ya Bill & Melinda Gates kwa uongozi wake katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto.
Chini ya uongozi wa Rais Samia, vifo vya kina mama vimeripotiwa kushuka kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi karibu vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000, mabadiliko ambayo wataalamu wa afya wanayataja kuwa ya kihistoria.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa mafanikio kama hayo katika afya ya mtoto yatakuwa magumu kufikiwa bila uwekezaji mahsusi katika kuongeza idadi ya madaktari bingwa wa watoto.
Wataalamu wa afya wanasema vyuo na vyuo vikuu vinapaswa kufanya zaidi kuwahamasisha madaktari vijana kubobea katika magonjwa ya watoto, taaluma ambayo mara nyingi huonekana kuwa ngumu na isiyo na vivutio vya kifedha ikilinganishwa na fani nyingine.
Akizungumza katika mahafali hayo, Rais wa AKU, Dk Sulaiman Shahabuddin, amesema chuo kimejikita katika kuboresha ubora wa maisha kupitia elimu, utafiti na huduma kwa jamii.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, AKU imeanzisha programu 18 mpya za shahada, zikiwemo kadhaa Afrika Mashariki, na programu ya magonjwa ya watoto iliundwa mahsusi kukabiliana na mahitaji ya kitaifa ya rasilimali watu,” amesema.