
Mbeya. Mambo yanazidi kuiendea vibaya Tanzania Prisons kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya leo Februari 10, 2026 kupokea kichapo kizito cha mabao 4-1 nyumbani kutoka kwa Coastal Union.
Kichapo hicho ambacho Tanzania Prisons imekipata katika Uwanja wa Sokoine, kimeifanya timu hiyo kubaki katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi zake tisa ilizokusanya katika mechi 12.
Hali inaweza kuwa ngumu zaidi kwa Tanzania Prisons ikiwa KMC itaibuka na ushindi katika mechi ya kesho dhidi ya Simba kwani itashuka kwa nafasi moja hadi mkiani mwa msimamo wa ligi.
Mabao manne ya Coastal Union katika mchezo wa leo yalipachikwa na Bakari Msimu aliyefunga mawili huku mengine yakiwekwa kimiani na Shiza Kichuya na Cleophace Mkandala wakati bao pekee la Tanzania Prisons lilifungwa na George Mpole.
Kwa kupoteza leo, Tanzania Prisons imeendeleza nuksi ya kutofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo imefikisha mchezo wa nane mfululizo kucheza bila kupata ushindi.
Timu hiyo imefikisha siku 124 bila kupata ushindi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwani tangu ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, Oktoba 21, 2025, imetoka sare katika michezo mitatu iliyofuata na kupoteza mitano.
Kwa upande wa Coastal Union, ushindi wa leo umeiwezesha kupanda kwa nafasi nne kwenye msimamo wa ligi ambapo kwa sasa ipo nafasi ya tisa ikifikisha pointi 14.
Baada ya ushindi wa leo, kibarua kinachofuata kwa Coastal Union ni dhidi ya JKT Tanzania, mechi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Meja jenerali Isamuhyo, Ijumaa wiki hii na Jumamosi, Tanzania Prisons itaialika Namungo FC.