Mchezaji wa Everton anayekipiga kwa mkopo kutokea Manchester City, Jack Grealish, amethibitisha kuwa msimu wake umefikia tamati baada ya kufanyiwa upasuaji wa jeraha la mguu lililovunja matumaini yake ya kushiriki Kombe la Dunia la msimu huu wa joto.

Grealish (30) awali ameripotiwa kupata maumivu yanayodhaniwa kuwa ya misuli ya paja lakini baada ya vipimo zaidi, imebainika kuwa alikuwa amepata mpasuko kwenye mguu, hali inayolazimu kufanyiwa upasuaji.

Kupitia ujumbe aliouchapisha akiwa kwenye kitanda cha hospitali, Grealish amewashukuru mashabiki wa Everton kwa sapoti kubwa waliompa tangu ajiunge na klabu hiyo.

Grealish amewashukuru mashabiki wa Everton kwa sapoti kubwa waliompa tangu ajiunge na klabu hiyo. Picha na Mtandao

“Sikutamani msimu uishe kwa namna hii, lakini huo ndiyo mpira wa miguu. Nimeumizwa sana,” ameandika Grealish.

“Upasuaji umekamilika na sasa nguvu zote ni kurejea nikiwa fiti. Nitarejea nikiwa imara zaidi kuliko awali.”

Mchezaji huyo amesisitiza mapenzi yake kwa Everton, akiwapongeza wafanyakazi, wachezaji wenzake na mashabiki kwa sapoti yao kubwa, huku akiahidi kuendelea kuwaunga mkono wenzake hadi atakaporejea uwanjani.

Jeraha hilo limefuta kabisa matumaini ya Grealish kuingia kwenye kikosi cha England kinachoandaliwa na Thomas Tuchel kwa ajili ya Kombe la Dunia litakalochezwa mwaka huu Marekani, Canada na Mexico.

Kocha wa Everton, David Moyes, amefichua kuwa Grealish anatarajiwa kubaki klabuni hapo kwa ajili ya matibabu na mazoezi ya kurejea uwanjani, badala ya kurejea klabu yake mama ya Manchester City.

Grealish anatarajiwa kubaki Everton kwa ajili ya matibabu na mazoezi ya kurejea uwanjani msimu ujao. Picha na Mtandao

Licha ya jeraha hilo, Everton bado wanaonesha nia ya kumsajili Grealish moja kwa moja dirisha la usajili lijalo la kiangazi.

Katika msimu huu, Grealish amecheza mechi 22 akiwa Everton, akifunga mabao mawili na kutoa pasi sita za mabao.

Baada ya taarifa za jeraha hilo, Everton wamemsajili kwa mkopo winga wa Chelsea, Tyrique George, hadi mwisho wa msimu.

Grealish pia amepata jumbe nyingi za kumtakia nafuu kutoka kwa mastaa mbalimbali wakiwemo Erling Haaland, Harry Maguire, Declan Rice, James Maddison na Curtis Jones, miongoni mwa wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *