
Idara ya Intelijinsia na Usalama wa Taifa ya Somalia (NISA) leo Jumanne imetangaza kuuawa kiongozi wa ngazi ya juu wa wanamgambo wa kundi la al- Shabaab katika oparesheni ya usalama.
Mohamed Sahal Idle, anayejulikana kwa jina maarufu Abu Usaama, ameuawa katika operesheni iliyofanywa kwa ushirikiano na washirika wa kimataifa karibu na mji wa Sakow, katika eneo linaloshikiliwa na al-Shabaab la Juba ya Kati.
Taarifa ya Idara ya Intelijinsia na Usalama wa Taifa ya Somalia imeongeza kuwa, Usaama alifahamika pakubwa kwa jinai zake dhidi ya wananchi wa Somalia na alikuwa mshirika wa karibu wa Ahmed Diriye kiongozi wa kundi la al Shabaab.
Mohamed Sahal Idle au Abu Usaama alikuwa akitayarishwa kuchukua nafasi ya mkuu wa zamani wa masuala ya fedha wa kundi hilo, Abdullahi Wadaad, aliyeuawa katika operesheni iliyoongozwa na Idara ya Intelijinsia na Usalama wa Taifa ya Somalia katika eneo la Kuunyo Barrow, katika jimbo la Lower Shabelle, Januari mwaka huu.
Taarifa ya Idara ya Intelijinsia na Usalama wa Taifa ya Somalia imeeleza kuwa Abu Ussama alihusika katika unyang’anyi na uporaji wa mali za raia wa Somalia.
Kundi la al Shabaab limethibitisha katika taarifa yake kwamba Mohamed Abu Usaama ameuawa katika shambulio la anga nje kidogo ya mji wa Sakow.
Kundi hilo la kigaidi lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi na hujuma mbalimbali dhidi ya serikali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 16 sasa, mara nyingi likiwalenga askari usalama, maafisa na raia wa kawaida.