Makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina yamesisitiza ulazima wa kukabiliana na mipango ya Wazayuni wenye misimamo mikali katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mustafa al Barghouthi ambaye ni Katibu Mkuu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina amesema: Wazayuni maghasibu wamejenga  mamia ya vitongoji vya walowezi na kuweka maelfu ya vituo vya ukaguzi vya kijeshi, ili kubadilisha taswira asilia ya ardhi ya Palestina na kuunganisha kikamilifu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Mustafa al Barghouthi

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) pia imesisitiza katika taarifa yake kuwa maamuzi haramu yaliyochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu Ukingo wa Magharibi hayaupi haki yoyote utawala huo ghasibu. 

Abu Samer Musa mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina pia amesisitiza kwamba kuna udhaura wa kuanzisha uratibu na kuwepo mshikamano kati ya Palestina na ngazi ya kimataifa ili kukabiliana na mipango haramu ya utawala ghasibu wa Israel. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina pia imetangaza kuwa hatua ya baraza la usalama la utawala ghasibu wa Israel ya kukubali mapendekezo ya Israel Katz na Bezalel Smotrich, mawaziri wa vita na fedha wa Israel, kuhusu ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika eneo la Ukingo wa Ukingo wa Magharibi, haikubaliki. 

Gazeti la Kizayuni la Yediot  Aharonoth pia huko nyuma liliripoti kuwa Israel Katz na Bezalel Smotrich wamechukua hatua za kuidhinisha msururu wa maamuzi ya kuimarisha unyakuzi na kuunganishwa kivitendo ardhi za eneo la Ukingo wa Magharibi na maeneo yaliyotwaliwa ya Palestina na kupachikwa jina la Israel.  

Makundi ya muqawama ya Palestina pia yamepinga kadhia hiyo kupitia taarifa yao ya pamoja na kusisitiza kuwa maamuzi mapya ya baraza la usalama la utawala ghasibu ya kupasisha kutwaliwa ardhi za Ukingo wa Magharibi yana maana ya kuliunganisha kivitendo eneo hilo na Israel, kulazimisha hali mpya na kuhitimisha  uwepo wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Makundi hayo ya Palestina yameongeza kuwa: Maamuzi mapya ya baraza la usalama lenye misimamo mikali la Israel ni sawa na kutangaza vita kupitia kuzidisha mchakato wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kubomoa nyumba za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na huko Quds; na ni kukanusha uwepo kisiasa Palestina na namna Israel inavyotekeleza hujuma hizo za kughusubu ardhi za Ukingo wa Magharibi kwa kutumia kifuniko cha mfumo wa kisheria na kiutawala. 

Makundi ya mapambano ya Palestina yanapinga sera za Israel za kutwaa ardhi za Ukingo wa Magharibi.

Mpango mpya wa Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada katika baraza la mawaziri la Netanyahu unauruhusu utawala wa Kizayuni kuharibu maeneo mbalimbali ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi. Kutekelezwa maamuzi hayo kutapelekea kupanuliwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Jibu la pamoja la makundi ya Kipalelestina kwa mpango mpya wa Wazayuni wenye misimamo mikali katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umejikita katika mambo kadhaa ya kisiasa, kitaifa na kistratijia. Mpango huu, khususan baada ya uamuzi wa baraza la mawaziri la usalama la utawala wa Kizayuni wa kupanua udhibiti wa Maeneo A na B ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan (ambao kwa mujibu wa Makubaliano ya Oslo, yanapaswa kuwa chini ya uongozi wa Palestina), unaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni unafuatilia kuendeleza  ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa kukiuka makubaliano ya zamani na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Mipango mipya katika baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni, hususan kupasisha unyakuzi wa maeneo A na B ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, haiishii kwenye “vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Katika fremu ya mpango huo, Wazayuni wana lengo na njama ovu ya kuunganisha hatua kwa hatua maeneo hayo na Israel. 

Umoja na mshikamano wa makundi ya Kipalestina dhidi ya mipango hiyo ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan sio tu ni jibu la kimbinu la muda mfupi, bali ni unadhihirisha uelewa mpana na wa pamoja wa tishio lililopo dhidi ya uwepo wa kitaifa na kijiografia wa Palestina.

Msimamo huo wa pamoja na mshikamano wa makundi ya Kipalestina unaonyesha ulazima wa kukabiliana na mipango ambayo inalenga sio tu ardhi bali pia utambulisho na mustakabali wa kisiasa wa watu wa Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *