Zanzibar. Mwanamuziki wa Singeli Amani Hamisi ‘Man Fongo’ anasema muziki huo ndiyo unaweza kulea Grammy nchini kutokana na midundo yake kuwagusa watu wengi.
Man Fongo ambaye ni mmoja kati ya wasanii waliotumbuiza kwenye jukwaa la Sauti za Busara 2026, amesema Singeli ikipigwa kila mmoja hucheza kwa kabila lake.
Picha ya mwanamuziki Man Fongo
“Grammy inawezekana kwa sababu Singeli haufanani na miziki mingine ya nje. Utabaki kuwa wa kwetu na ikipigwa watu wa makabila yote wanacheza. Kwasababu inaingiza muziki wa kabila zote Tanzania.
“Ni mara yangu ya kwanza kutumbuiza Sauti za Busara nimejisikia vizuri sana, kwasababu fursa hizi watu wengi wanaziota. Lakini hawazipati, nikaona nioneshe uwezo wangu hili ni tamasha la kimatafa. Nikafanya kama ambavyo huwa nafanya kwenye shoo zangu nje ya nchi,”amesema
Kupitia jukwaa hilo Man Fongo alipiga muziki wa Singeli live, huku kukiwa na upigwaji wa ala mbalimbali za muziki.
“Uzoefu huu nimeupata kwa sababu ya shoo zangu za Ulaya, Tumepiga live bila DJ ili kujenge muziki msafi zaidi,”amesema.
Man Fongo akiwa kwenye akitumbuiza kwenye jukwaa la Sauti za Busara, Februari 6,2026
Licha ya kuwa baadhi ya wasanii huwa na sifa ya kutodumu kwenye uhusiano Man Fongo anasema yake yana miaka 12 sasa.’
“Shemeji yenu tumefikisha mwaka wa 12 sasa. Siri ni kupendana na kuvumiliana vizuri vipo vingi wapo wanaotupenda na kututamani lakini heshima ikibaki mtadumu.
“Kuna vitu tunaweza kufanya ikawa siri yetu. Lakini unakuwa unajua fulani ni mke wangu ukirudi nyumbani heshima yake inabaki palepale,”anasema Man Fongo