
Ukarabati wa Soko Kuu la Kariakoo kwa gharama ya Sh28 bilioni ni ushahidi wa dhamira ya Serikali kuboresha miundombinu ya biashara na kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara.
Tunaamini uwekezaji huu mkubwa ni hatua sahihi kuelekea kulifanya soko hilo kuwa la kisasa na lenye hadhi ya kikanda.
Hata hivyo, thamani ya uwekezaji huo haitapimwa kwa majengo ya kisasa pekee, bali kwa ufanisi wa mifumo ya usimamizi, hasa katika ukusanyaji na matumizi ya mapato.
Bila usimamizi thabiti wa mapato, soko hilo linaweza kurejea katika changamoto zilezile zilizolisumbua kabla ya kuungua moto, ikiwamo uchakavu wa miundombinu, uchafuzi wa mazingira na misongamano isiyodhibitiwa.
Mapato yanayotokana na kodi za vizimba, tozo za huduma na ada mbalimbali ndizo mhimili wa uendelevu wa soko. Mapato hayo yanapaswa kuonekana wazi, kukusanywa kwa mifumo ya kidijitali na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Uwazi huu utapunguza mianya ya ubadhirifu na kuongeza imani ya wafanyabiashara kwa uongozi wa soko. Pale mapato yanapokusanywa kwa uwazi, inakuwa rahisi kupanga matengenezo ya miundombinu muhimu kama mifumo ya majitaka, maji taka na zimamoto, ambayo ni nguzo ya usalama na afya ya umma.
Suala la mazingira nalo linahitaji kupewa kipaumbele cha juu, kwani soko lisiposimamiwa vyema litakuwa kitovu cha mrundikano wa takataka na uchafu, hali itakayotishia afya za wafanyabiashara na wateja.
Ni muhimu mapato ya soko kuelekezwa katika mifumo endelevu ya ukusanyaji na usafishaji wa taka, pamoja na matengenezo ya mifumo ya majitaka ili kuzuia mafuriko, harufu mbaya na magonjwa.
Usafi wa mara kwa mara, uwekaji wa vyombo vya kutupia taka na mikataba ya uhakika na wakusanyaji wa taka ni hatua zinazopaswa kuwa sehemu ya mpango wa kudumu, si wa msimu.
Hakuna sababu ya kurudi nyuma katika udhibiti huu, kila kipengele cha soko lazima kiwe na uwajibikaji dhahiri, ili Kariakoo iendelee kuwa soko la mfano kwa taifa na kikanda.
Pia, changamoto ya maegesho ya magari iliyowahi kulisonga Kariakoo kwa miaka mingi haipaswi kuruhusiwa kurejea. Tunasema kwa msisitizo usimamizi mzuri wa utaratibu wa maegesho na njia za kupakia na kupakua mizigo ni muhimu ili kulinda mtiririko wa biashara na usalama wa watumiaji wa soko.
Mapato yatokanayo na huduma za maegesho yakisimamiwa kwa uwazi, yanaweza kutumika kuboresha miundombinu ya barabara za ndani, alama za maegesho na ulinzi, hivyo kuondoa vurugu na msongamano.
Hivyo, uongozi wa soko, Tamisemi na mamlaka za jiji wanapaswa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mifumo ya kisasa ya mapato, kuhakikisha ukaguzi wa mara kwa mara, uwajibikaji wa kila sehemu, uwazi katika ukusanyaji na matumizi, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa sera na mipango yote inayohusiana na soko.
Soko la Kariakoo ni moyo wa biashara ya jiji na kikanda, uhai wake utategemea si uzuri wa majengo, bali nidhamu ya usimamizi wa mapato na matumizi yake kwa maendeleo endelevu ya mazingira, miundombinu na huduma kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.