Iran haitasalimu amri wala kukubali mashinikizo au masharti ya Marekani huku ikiendelea na mazungumzo na Washington, amesema Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi, msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran, katika mahojiano maalum na Press TV.

Kauli hiyo imekuja kufuatia duru mpya ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya wawakilishi wa Iran na Marekani, yaliyofanyika Ijumaa mjini Muscat, Oman.

Jenerali Shekarchi amesisitiza kuwepo kwa uratibu na mshikamano kati ya vyombo vya kijeshi na kidiplomasia vya Iran, akihimiza timu ya diplomasia kuendelea na mazungumzo kwa msimamo thabiti, kwa kuwa inaungwa mkono na taifa pamoja na Vikosi vya Ulinzi.

Ameongeza kuwa: “Sisi kama Vikosi vya Ulinzi vya Iran, tuko tayari kukabiliana na mpango wowote unaoweza kupangwa na Marekani dhidi ya nchi yetu, na tutajibu ipasavyo, kwa wakati unaofaa.”

Akijibu swali kuhusu kiwango cha utayari wa kijeshi na uwezo wa kuzuia (deterrence) wa Iran, Jenerali Shekarchi amesema kuwa Iran iko katika “ngazi ya juu sana” ya tahadhari ili kukabiliana na hatua zozote za maadui.

Amesema tangu vita vya siku 12, Vikosi vya Ulinzi vimekuwa vikiongeza kiwango cha utayari wake ili kukabiliana na “kosa lolote la kimkakati” kutoka kwa maadui.

Amesema Vikosi vya Ulinzi vya Iran sasa viko katika hali ya juu zaidi ya utayari kuliko ilivyokuwa awali.

Jenerali Shekarchi amesisitiza tena dhamira ya vikosi hivyo kulilinda taifa na mipaka ya Iran, pamoja na kuimarisha uwezo wa mashambulizi, iwapo kutatokea makadirio potofu kutoka kwa maadui.

Aidha, ametoa onyo kali kwa Marekani na Israel dhidi ya hatua yoyote mpya ya uchokozi, akisema majibu yatakuwa makali zaidi na ya maamuzi.

Msemaji huyo ameonya kuwa maslahi ya Marekani na Israel katika ukanda mzima yatawekwa hatarini.

Amesema:“Tutapanua malengo yetu zaidi ya yale yaliyolengwa wakati wa vita vya siku 12, ikiwemo maslahi yao ya kiuchumi. Tutasababisha matatizo ya kiuchumi kwa Marekani.”

Jenerali huyo ameongeza kuwa mtu au nchi yoyote itakayoungana na Marekani katika kosa lolote la kimkakati dhidi ya Iran itaongezwa katika orodha ya malengo ya Iran.

Ameapa kuwa Marekani na Israel watalipa gharama ya kosa lolote jipya, akisema:
“Wakati wa vita vya siku 12, walipata pigo kubwa sana kutoka upande wa Iran, na safari hii litakuwa kubwa zaidi, zito zaidi.”

Mnamo Juni 24, Iran, kupitia operesheni za kijeshi zilizokuwa na mafanikio za kujibu uchokozi wa utawala wa Israel na Marekani, ilifanikiwa kulazimisha maadui hao kusitisha uchokozi huo haramu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *