Riyadh, Saudi Arabia. Cristiano Ronaldo amemaliza mgomo wake ndani ya Klabu ya Al-Nassr baada ya uongozi wa timu hiyo kukubali baadhi ya matakwa yake muhimu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Ureno, nyota huyo anayekadiriwa kulipwa zaidi ya Pauni 488,000 kwa wiki, amekosa mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu ya Saudi Arabia kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa klabu, hususan ukosefu wa nguvu ya kifedha katika dirisha la usajili.

Ronaldo (40) ameripotiwa kukasirishwa na hatua ya wapinzani wao Al-Hilal kumsajili aliyekuwa mchezaji mwenzake Real Madrid, Karim Benzema, huku Al-Nassr wakishindwa kufanya usajili mkubwa zaidi ya kuongeza mchezaji mmoja kijana.

Mshambuliaji mpya wa Al-Hilal, Karim Benzema. Picha na Mtandao

Kwa mujibu wa gazeti la A Bola kutoka Ureno, Al-Nassr sasa wamewarudishia mamlaka baadhi ya viongozi wakuu akiwemo Jose Semedo, rafiki wa karibu wa Ronaldo, pamoja na Simao Coutinho, jambo linalodaiwa kumfurahisha nahodha huyo wa zamani wa Manchester United.

Mbali na hilo, Ronaldo pia amelalamikia kutokuwepo kwa usawa ndani ya klabu, ikiwemo madai ya kucheleweshwa mishahara ya baadhi ya wafanyakazi, hali iliyosababisha uongozi kulipa madeni hayo ili kurejesha hali ya utulivu.

Ingawa amerejea mazoezini, Ronaldo hakusafiri na kikosi kwenda kwenye mchezo wa Kombe la Klabu Bingwa Asia (AFC) dhidi ya Arkadag ya Turkmenistan, badala yake anatarajiwa kurejea uwanjani Jumamosi dhidi ya Al-Fateh ligi itakaporejea.

Ronaldo anatarajiwa kurejea uwanjani Jumamosi Februari 14, 2026  katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Al-Fateh. Picha na Mtandao

Cha kushangaza, Al-Nassr wameshinda mechi zote mbili alizokosa Ronaldo ikiwemo ushindi wa 2-0 dhidi ya Al-Ittihad hali iliyozua mjadala mpana kuhusu utegemezi wa timu hiyo kwa nyota huyo.

Hata hivyo, uongozi wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia umepuuza madai ya Ronaldo, ukisisitiza kuwa kila klabu inafanya maamuzi yake kwa uhuru na hakuna mchezaji mmoja aliye juu ya mfumo.

Tangu ajiunge na Al-Nassr Januari 2023, Ronaldo bado hajafanikiwa kushinda taji kubwa lolote, huku akizidiwa na wapinzani wao wakuu Al-Hilal na Al-Ittihad.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *