
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Neema Nyamwaka akizungumza baada ya kupokea vifaa amesema, “hivi tunasema asante kwa sababu ya kutukumbuka leo kuja kuongea na watoto na kuja kututazama. Tunashukuru kwa sababu nyie watanzania kutukumbuka kila mara. Miaka iliyopita tulikuwa na wageni hapa watanzania tu. Tunasema asante kwa kuwa mnatakumbuka.”
Kwa Matabashi Belungu, Mwalimu katika shule ya msingi Ngite anakumbuka usaidizi wa kufundisha walimu jinsi ya kutumia kompyuta, halikadhalika hospitali na taa za barabarani. “Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea mema,” amesema Mwalimu Belungu.
Miongoni mwa vifaa walivyopatiwa ni madaftari na vitabu ambapo Clarice Masika, Mwalimu pia katika shule hii ya msingi anasema, “tunajitahidi ili watoto wafahamu kile tunachosema pia waelewe lugha yetu ambayo tunafundisha hapa shuleni. Changamoto ambayo tunakutana nayo kwa watoto unaona kuna wakati mtoto anakuja bila madaftari.”
Naye Mwakilishi wa masuala ya jinsia kutoka Tanzania, Sharifa Omar ameeleza kuwa TANZBATT12 itaendeleza ushirikiano zaidi kwa kuzifikia shule mbali mbali ndani ya mji wa Beni.
Amesema, “siku ya leo tumefika katika shule hii ambayo ipo katika mji wa Beni na tumekuja na baadhi ya vifaa ambavyo vitawasaidia katika masomo yao. Tunaenda katika shule mbalimbali na chochote ambacho tutakuwa nacho, tutakuwa tunasaidiana nao ili kuendeleza ushirikiano.”