
Hatua ya Serikali kutangaza mpango wa kuiboresha Barabara ya Mandela kuanzia kivuko cha Kijazi hadi Daraja la Nyerere Kimbano sambamba na kuimarisha njia za kuingia na kutoka Bandari ya Dar es Salaam inakwenda kutatua kilio cha muda mrefu kuhusu kero ya foleni.
Mradi huo wa ujenzi wa Barabara ya Mandela ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hususan kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hiyo kama njia kuu inayoelekea bandarini.
Tunatambua bandari ni mhimili wa biashara, usafirishaji wa bidhaa, na mapato ya taifa; hivyo basi, barabara inayohudumia bandari inapaswa kupewa kipaumbele cha juu ili kuhakikisha shughuli zote zinazohusiana na uingizaji na usafirishaji wa mizigo zinafanyika kwa ufanisi.
Kukamilika kwa haraka kwa ujenzi wa Barabara ya Mandela kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa magari, ambao kwa muda mrefu umekuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara, madereva wa malori, na wananchi kwa ujumla. Foleni ndefu husababisha upotevu wa muda, ongezeko la gharama za usafirishaji, matumizi makubwa ya mafuta, pamoja na uchovu kwa watumiaji wa barabara.
Zaidi ya hapo, ucheleweshaji wa mizigo bandarini huathiri ushindani wa bandari yetu ikilinganishwa na bandari nyingine za kikanda. Kukamilika kwa mradi huu kwa wakati kutaimarisha ufanisi wa bandari na kuongeza imani ya wawekezaji na wafanyabiashara.
Aidha, barabara hii ina mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa kufungua fursa za ajira wakati wa ujenzi na baada ya kukamilika.
Vijana wengi watanufaika kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, huku sekta nyingine kama biashara ndogo ndogo, usafirishaji, na huduma zikipata msukumo mkubwa wa ukuaji. Kwa mantiki hiyo, kasi ya ujenzi inapaswa kuzingatiwa kwa umakini mkubwa, bila kuathiri ubora na viwango vinavyotakiwa.
Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa kukamilisha mradi kwa haraka, ni lazima maandalizi ya kina yafanyike ili kudhibiti changamoto za foleni zitakazojitokeza wakati wa ujenzi.
Ni muhimu kuwepo kwa njia nyingi na tofauti za mchepuko zitakazowezesha magari kupita bila kusababisha msongamano mkubwa. Njia hizi zinapaswa kupangwa kwa kuzingatia aina tofauti za magari, hususan malori makubwa yanayoelekea au kutoka bandarini, magari ya abiria, pamoja na usafiri wa umma.
Vilevile, mamlaka husika zinapaswa kutoa taarifa kwa umma mapema kuhusu njia za mchepuko, ratiba za ujenzi, na maeneo yatakayofungwa kwa muda.
Utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati utasaidia madereva kupanga safari zao mapema na hivyo kupunguza usumbufu usio wa lazima.
Matumizi ya alama za barabarani zinazoeleweka, askari wa usalama barabarani, pamoja na teknolojia za kisasa za usimamizi wa trafiki ni mambo muhimu yatakayosaidia kudhibiti foleni wakati wa utekelezaji wa mradi.
Barabara ya Mandela ni mradi wa msingi unaogusa maisha ya wananchi wengi na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Ni muhimu kuwepo wa njia mbadala nyingi na mipango madhubuti ya usimamizi wa trafiki wakati wa ujenzi ni muhimu ili kuhakikisha shughuli za kila siku zinaendelea bila usumbufu mkubwa.