GEITA: WACHIMBAJI wadogo wa mgodi wa Msasa kijiji cha Msasa kata ya Runzewe-Magharibi wilayani Bukombe wamejitolea kukamilisha zahanati ya kijiji hicho iliyokwama kwa zaidi ya miaka 10.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Msasa, Cosmas Ignasi ametoa taarifa hiyo mbele ya viongozi wa serikali ya kijiji walipofika kutembelea na kukagua maendeleo ya zahanati hiyo.

Ignasi amesema uongozi wa Mgodi huo umewiwa kuikamilisha zahanati hiyo baada ya kusikia kilio cha wakazi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Amesema ukamilishaji wa zahanati hiyo ni sehemu ya kurejesha kwa jamii kwa kutambua kuwa wao kama wachimbaji wadogo wamepata riziki yao kwenye eneo lililopo ndani ya kijiji hicho.

“Sisi malengo yetu ni kuhakikisha tunalijenga jengo mpaka tunalimaliza na kuikabidhi serikali likiwa limekamilika na kutoa nafasi kwa serikali kuleta vifaa pamoja na watoa huduma.

“Tumejipanga kuhakikisha tunapoondoka Msasa tuache alama kubwa na tumejidhatiti kushirikiana na viongozi wa eneo husika kwa changamoto yeyote inayotokea tuweze kuchangia.

Ofisa Tarafa ya Siloka, Zuhura Kashindi amesema mbali na wakazi wa Msasa pia zahanati hiyo inaenda kuwa msaada wa watu wengi ambao wamekuja eneo la Msasa kwa ajili ya uchimbaji.

Zuhura amesema mgodi huo umeongeza idadi ya watu kwenye kijiji cha Msasa na tarafa ya Siloka na hivo kuongeza mahitaji ya huduma za kijamii pamoja na mapato ya halmashauri ya Bukombe.

“Wananchi wa Kijiji cha Msasa walikuwa wanaenda kata ya Uyovu na Runzewe Mashariki kufuata huduma ya afya lakini uwepo wa zahanati kwenye eneo la oni msaada mkubwa”.

Ofisa Mtendaji wa kata ya Runzewe-Magharibi, Beatrice Nehemia amesema ufadhili wa wawekezaji wa mgodi wa Msasa unahusisha upauaji na ukamilishaji wa boma la zahanati lote.

Amesema ufadhili huo utapunguza changamoto ya huduma za afya ndani ya kata ya Runzewe Magharibi kwani wananchi wake wengi wamekuwa wakilazimika kufuata huduma kata za jirani.

Mwenyekiti wa kijiji cha Msasa, Tulinge Paschal amesema ujenzi wa zahanati hiyo ulianza miaka 10 iliyopita kupitia nguvu za wananchi kuanzia hatua ya msingi mpaka ujenzi wa boma.

Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kijiji cha Msasa, Salustia Adam amekiri kuwa wajawazito wengi walikuwa wanashindwa kuhudhuria kliniki kutokana na huduma za afya kupatikana kata Jirani.

Amesema zahanati hiyo itapunguza adha ya kina mama, wazee na watoto kupoteza maisha kwa kukosa huduma ya kwanza badala yake watapata uhakika wa huduma ya afya kwenye eneo lao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *