Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba leo Jumanne, Februari 10, 2026 amekutana na Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) kwa ajili ya kupitia hatua mbalimbali zilizofikiwa katika maandalizi ya michuano hiyo itakayofanyika mwakani katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Mwigulu amefanya kikao hicho katika Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu amepongeza kazi kubwa inayofanywa na kamati hiyo, akieleza kuridhishwa na kasi na mwelekeo wa maandalizi yanayoendelea.
“Maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa yanaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji bora wa michuano hiyo,”.amesema Mwigulu.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ni muhimu kuwepo kwa ushirikishwaji wa sekta zote.
“Mawaziri, makatibu wakuu pamoja na watendaji wengine hakikisheni mnazishirikisha sekta zetu kila mmoja katika eneo lake, tunataka kuona matokeo chanya katika michuano hii,” amesema Mwigulu..
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuhakikisha kila mmoja anasimamia kikamilifu eneo lake la uwajibikaji, ili hatua zote za maandalizi zikamilike kwa muda uliopangwa na kwa viwango vinavyokubalika.
Fainali za AFCON 2027 zimepangwa kufanyika mwakani kuanzia Juni 19 hadi Julai 14 zikishirikisha timu za taifa 24 zitakazogawanywa katika makundi sita yenye timu nne kila moja.
Toleo hili la mashindano litakuwa la kwanza kuandaliwa kwa pamoja na nchi tatu, na pia la kwanza kufanyika katika ukanda wa CECAFA baada ya kipindi cha zaidi ya miongo mitano, tangu Ethiopia ilipoandaa mashindano hayo mwaka 1976.
Mashindano haya ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Pia yatakuwa ya mwisho kufanyika kila baada ya miaka miwili, baada ya CAF kutangaza kwamba kuanzia mwaka 2028, AFCON itakuwa ikifanyika kila baada ya miaka minne.
Senegal ndiyo mabingwa watetezi.ambao walitwaa taji hilo, Januari 18, 2026 kwa kuifunga Morocco kwa bao 1-0 katika fainali.