Wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliohudhuria maandamano ya Bahman 22 mjini Tehran wameidhinisha azimio la maandamano hayo na kutangaza kwamba, sasa ni wakati wa ushirikiano kati ya medani ya kijeshi na ya diplomasia, na kwamba askari wa nyuga zote hizo mbili wanatokana na kizazi cha taifa na wanaungwa mkono kwa asilimia mia moja na wananchi wa Iran.
Azimio rasmi la maandamano ya tarehe 22 Bahman limesema: Katika kumbukumbu ya miaka 47 ya ushindi wenye adhama wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, taifa adhimu, lenye uelewa, basira, na linalojitokeza kila wakati katika medani ya harakati la Iran ya Kiislamu, kwa mara nyingine tena limejitokeza kwa uelewa wa kumvunja nguvu adui, kwa uwezo na nguvu kamili, na kwa namna inayojenga izza na heshima katika maandamano ya nchi nzima ya Siku ya Allah ya tarehe 22 Bahman, ili kusisitiza na kutilia mkazo kushikamana kwake kwa dhati na kusikoweza kuyumbishwa na malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu, fikra zing’arazo za Imam Khomeini (MA) akiwa ndiye msanifu mkuu wa harakati hiyo ya kidini, na miongozo ya hekima na ya kimkakati ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Imam Khamenei (Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu).
Azimio hilo limesema: Mahudhurio haya yenye adhama na ya kujenga umoja ni dhihirisho la wazi la ukomavu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa, na umakini wa kihistoria wa taifa la Iran dhidi ya njama tata, mashinikizo yanayoongezeka, na vita mseto vya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu, hususan Marekani na utawala wa Kizayuni pamoja na washirika wao; vita ambavyo -katika kipindi cha karibuni, kutokana na uvamizi wa wazi na vita vya kulazimisha vya siku 12 dhidi ya taifa la Iran na kambi ya Muqawama, pamoja na matukio machungu ya jaribio la mapinduzi la Marekani na Kizayuni lililotekelezwa na mamluki wao wa kigaidi wenye silaha-, vimezidi kufichua sura halisi ya uadui, ukatili, na ya kutapatapa ya mfumo wa ubeberu, na wakati huo huo, vimewathibitishia walimwengu uthabiti na kusimama imara kwa taifa la Iran na Mhimili wa Muqawama ikiwa ni hakika isiyoweza kukanushika.

Azimio hilo la Bahman 22 la mwaka huu wa 1404 Hijria Shamsia limeashiria misimamo na matakwa ya washiriki wa maandamano hayo ya kitaifa nchini kote na kueleza: “Sisi wananchi wa Iran, tunawaunga mkono askari wa diplomasia na askari wa medani ya vita; na katika mazingira nyeti na hasasi ya sasa tunasisitiza kwamba, tunaunga mkono majadiliano na mazungumzo yoyote yale yanayofanyika chini ya misingi mikuu inayozingatia “heshima, hekima, na maslahi” na kutangaza uungaji mkono wetu imara kwa mihimili miwili hii ya nguvu na mamlaka ya nchi. Sasa ni wakati wa ushirikiano wa pamoja wa medani ya kijeshi na diplomasia, na askari wa medani zote mbili wanatokana na kizazi cha taifa na wanaungwa mkono na wananchi kwa 100%.”
Sehemu nyingine ya azimio la Bahman 22 imesema: Sisi, washiriki katika maandamano haya adhimu ya wananchi, tunavitambua vitendo vya kivamizi, vya kuvuruga uthabiti, na vya kijinai vya utawala wa Kizayuni na serikali ya Marekani kuwa ndio chanzo kikuu cha kukosekana usalama, kuzuka vita, na migogoro ya kila mara katika eneo hili. Na sambamba na kulaani vikali sera hizi za kinyama, tunasisitiza na kutangaza kwa mara nyingine tena kwamba kuna ulazima kwa fikra za umma ulimwenguni kuziwajibisha tawala hizi mbili kwa uhalifu na jinao zao dhidi ya mataifa madhulumu ya eneo hili, hasahasa wananchi imara wa Palestina na Ghaza. Na ni lazima uhalifu wa serikali ya Marekani katika fitna ya kigaidi ya mwezi Januari ufuatiliwe na taasisi zinazohusika…/