Onyo hilo la UN Women ni kali na linaungwa mkono na takwimu za miongo mitatu. Licha ya kuwa nusu ya idadi ya watu duniani, wanawake leo wanachangia asilimia 26 tu ya wahusika na vyanzo vya habari kimataifa, idadi ambayo imebadilika kidogo sana katika miaka 15 iliyopita.
Kwa mujibu wa utafiti wa Mradi wa Kufuatilia Vyombo vya Habari Duniani wa mwaka 2025 (GMMP), ambao ni utafiti wa muda mrefu zaidi duniani kuhusu sauti za wanawake kwenye habari, maendeleo katika uwakilishi wa kijinsia kwenye vyombo vya habari hayajakwama tu, bali yako hatarini.
Katika matangazo ya televisheni, redio na vyombo vya habari vya kuchapishwa, sauti za wanawake bado hazionekani kwa kiasi kikubwa, na uandishi wa habari unaopinga mitazamo potofu umeshuka hadi asilimia 2 tu ya habari zote.
Kalliopi Mingeirou (kulia), Mkuu wa Kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake katika UN Women, akihutubia tukio kwenye Kituo cha Haki cha City Bar huko New York. (Maktaba)
Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya Kihindi, Kalliopi Mingeirou, Mkuu wa kitengo cha kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake cha UN Women, ameeleza kuwa tatizo si ukosefu wa utaalamu kwa wanawake, bali ni mifumo ya zamani ya vyumba vya habari.
“Wanawake wanabaki kuwa mtu mmoja tu kati ya wanne wanaoonekana au kusikika kwenye habari… Hii ni kwa sababu tabia za vyumba vya habari na upendeleo havijabadilika. Vyombo vya habari vinaendelea kutegemea kundi lilelile la watu, mara nyingi vikiwachukulia wanaume kama wataalamu na wafanya maamuzi pekee”, amesema.
Vyombo vya habari vinaficha ukatili
Jambo linaloibua maswali zaidi ni jinsi ukatili wa kijinsia unavyofichwa, ambapo chini ya habari 2 kati ya 100 zinagusa dhuluma wanazofanyiwa wanawake.
“Ukatili dhidi ya wanawake unagusa nusu ya idadi ya watu, lakini hauzungumziwi kabisa habarini. Vyumba vya habari lazima vitambue kuwa hili siyo ‘suala la wanawake’ bali ni janga la kijamii linalohitaji kuonekana”, Mingeirou ameongeza.
Hata hivyo, kuna mkanganyiko kwani idadi ya waandishi wanawake imeongezeka hadi asilimia 41, kutoka asilimia 28 mwaka 1995 jambo linaloweza kubadilisha jinsi habari zinavyoandikwa lakini hali bado si yenye kuridhisha.
Ilianzishwa mwaka 2002, Khabar Lahariya, kihalisi news waves, ni shirika la vyombo vya habari la wanawake linaloendeshwa na waandishi wa habari wa vijijini, wengi wao ni wanawake wa Dalit, Adivasi na Waislamu.
Wanawake wanaleta mapinduzi katika habari
Nchini India katika maeneo ya vijijini, shirika la habari la wanawake pekee, Khabar Lahariya (Mawimbi ya Habari) limekuwa mfano wa kuigwa tangu mwaka 2002. Mwanzilishi wake, Kavita Devi, anakumbuka walivyodharauliwa mwanzoni.
“Tulikumbana na changamoto kila upande. Watu walisema wanawake hawawezi kuwa waandishi wa habari. Lakini tulienda vijijini, tukasimama imara, na tukathibitisha kuwa wanawake wanaweza kuripoti na kusimulia habari ambazo wengine hawawezi”, amesimulia.
Mmoja wa waandishi wa habari wa shujaa katika shirika hilo ni Shyamkali, ambaye hapo awali alikuwa hajui kusoma wala kuandika, lakini kwa sasa ni mwandishi mwandamizi anayetumia teknolojia ya kisasa. Akielezea safari yake ya mafanikio, Shyamkali anasema.
“Sikujua jinsi ya kuandaa wasifu au kushika kamera, lakini kwa mafunzo na maelekezo, nimeweza kujifunza kila kitu, kuanzia kuhoji hadi uandishi wa kutumia simu, na sasa ninaripoti habari ambazo vyombo vikubwa vinazipuuza”, amesimulia.
Khabar Lahariya inaripoti katika lugha za mashinani, Bundeli, Awadhi, Bhojpuri, ikikataa wazo kwamba uhalali unahitaji wasomi, Hindi ya mijini au Kiingereza.
Kwa kuhitimisha, Kirsi Madi amesisitiza hitaji la mabadiliko ya haraka ili kuipa dunia picha kamili ya maisha ya binadamu wote.
“Bila sauti za wanawake, hakuna habari iliyokamilika, hakuna demokrasia ya haki, hakuna usalama wa kudumu, wala mustakabali wa pamoja”