Dar es Salaam. Uhifadhi wa mazingira unaendelea kuwa ajenda muhimu duniani kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa ardhi na upotevu wa bayoanuwai.
Tafiti mbalimbali za kimataifa zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya uharibifu wa mazingira duniani unatokana na shughuli zisizo endelevu za kilimo, ikiwemo matumizi makubwa ya kemikali na ukataji miti ovyo.
Kutokana na hali hiyo, jitihada za kuhamasisha kilimo endelevu zimeendelea kuchukuliwa kama suluhisho muhimu la kulinda mazingira huku zikiimarisha usalama wa chakula na afya ya jamii.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Asasi ya AGENDA imetekeleza mradi wa kuhamasisha wakulima kutumia kilimo endelevu kinacholinda ardhi, maji na afya za walaji.
Katibu Mtendaji wa AGENDA, Dorah Swai, amesema asasi hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa mradi huo baada ya kufanya ziara ya ufuatiliaji iliyohusisha wakulima pamoja na shule za msingi na sekondari zilizopatiwa miche ya miti ya matunda.
Amesema mradi huo uliwalenga kuwahamasisha wakulima kuachana na matumizi ya viuatilifu vyenye kemikali kali na badala yake kutumia viuatilifu asilia vinavyotengenezwa kwa malighafi za asili kama majani ya mimea na mbinu nyingine rafiki kwa mazingira. Kwa mujibu wa wataalamu wa kilimo, matumizi ya kemikali nyingi kwenye udongo yanaweza kupunguza rutuba ya ardhi kwa muda mrefu, huku pia yakichafua vyanzo vya maji na kuathiri afya ya binadamu.
“Katika mradi huu tulikuwa tunahimiza wakulima kulima kilimo endelevu ambacho hakitumii kemikali za viwandani zenye sumu. Badala yake tumewaelekeza jinsi ya kutengeneza viuatilifu vya asili kwa kutumia majani na malighafi nyingine za asili,” amesema Swai.
Mbali na matumizi ya dawa asilia, wakulima walihamasishwa kupanda miti ya matunda mashambani na katika shule mbalimbali. Upandaji wa miti ni moja ya njia zinazotambulika kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwani mti mmoja uliokomaa unaweza kufyonza wastani wa kilogramu 20 za hewa ya ukaa kwa mwaka, hivyo kusaidia kupunguza ongezeko la gesi joto duniani. Aidha, miti ya matunda hutoa lishe bora, kivuli na chanzo cha kipato kwa wakulima na taasisi kama shule.
“Tuliwahamasisha kupanda miti ya matunda kwa sababu ina faida nyingi, ikiwemo chakula, kivuli na kusaidia kukabiliana na tabianchi,” amesema Swai.
Swai amesema tathmini ya awali inaonesha wakulima wengi walioshiriki mradi huo wameanza kuona manufaa ya moja kwa moja, ikiwemo kupungua kwa gharama za uzalishaji kutokana na matumizi ya pembejeo asilia pamoja na kuongezeka kwa ubora wa mazao. Ameongeza kuwa mradi huo pia umeunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa chakula mashuleni, kwani miti ya matunda iliyopandwa itakapokua itasaidia wanafunzi kupata lishe na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Kigamboni, Priscila Mhina, amesema halmashauri imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwafikia wakulima kwa mafunzo ya kilimo bora na kuwapatia ushauri wa kitaalamu kupitia maafisa ugani waliopo katika kata zote. Amesema elimu ya kilimo hai (organic farming) imekuwa msaada mkubwa kwa wakulima, kwani inalinda afya ya mlaji na mazingira kwa wakati mmoja.
“Kupitia mradi wa AGENDA tunawahamasisha wakulima kutumia dawa za asili kulinda ardhi na mazao, kwani kemikali nyingi huacha mabaki yenye sumu yanayoweza kumuathiri mlaji,” amesema Mhina.
Wakulima na walimu walionufaika na mradi huo wameeleza kuwa mafunzo waliyopata yamewasaidia kubadili mtazamo kuhusu kilimo, wakitambua kuwa kilimo kinacholinda mazingira si tu kinahifadhi rasilimali za asili bali pia kinaongeza tija na kipato chao kwa muda mrefu.
Kwa ujumla, wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa uwekezaji katika kilimo endelevu, upandaji miti na matumizi ya pembejeo rafiki kwa mazingira ni hatua muhimu katika kulinda rasilimali za taifa. Miradi kama huu wa AGENDA inaonesha namna ushirikiano kati ya Serikali, asasi za kiraia na wakulima unavyoweza kuleta matokeo chanya katika uhifadhi wa mazingira, usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi ya jamii.