Dar es Salaam. KMC itakuwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa KMC, Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam kukabiliana na Simba leo Februari 11, 2026 katika mechi ya Ligi Kuu itakayoanza saa 1:00 usiku.
Licha ya KMC kuonekana kutofanya vizuri katika michezo yao iliyopita, mchezo wa leo hautakuwa mwepesi kwa pande zote mbili kutokana na kila timu kuhitaji ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri katika msimamo wa ligi.
Hadi sasa vijana wa kocha, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ wameondoka na ushindi katika mechi mbili za ligi, wakipata sare mara mbili na kupoteza mechi 10 katika michezo 14 waliyocheza huku wakibuluza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Simba, wao wanatafuta ushindi ili kurudi katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi, ambapo imeshacheza mechi saba, ikishinda tano, ikitoa sare mechi moja na kupoteza moja huku ikishika nafasi ya saba ikiwa na pointi 16.
KMC ambao ni wenyeji wa mchezo huo, watakuwa na kazi kubwa kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza mbele ya Simba tangu timu hizo zianze kukutana katika michezo ya Ligi Kuu.
Winga wa KMC, Edson Mwijage, akijaribu kumtoka beki wa Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu iliyomalizika kwa sare ya 1-1Januari 27, 2026. Picha na KMC
Rekodi zinaonyesha kwamba, KMC iliyoanza kushiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19, haijawahi kushinda mbele ya Simba katika mechi 14 walizokutana kwenye Ligi Kuu.
Katika mechi hizo, imeshuhudiwa mara mbili pekee KMC ikiambulia sare tena zote ni matokeo ya 2-2, iliyopata Septemba 7, 2022 na Desemba 23, 2023.
Kabla ya hapo, Simba iliifunga KMC mechi nane mfululizo za ligi kabla ya kuwasimamisha mechi ya tisa ambayo waliambulia pointi ya kwanza kutokana na kupata sare. Kisha wakafungwa, halafu wakajiuliza tena na kuambulia sare, huku mechi tatu za mwisho wakifungwa tena 1-0, 4-0 na 1-2.
Ni mara moja pekee ambayo mchezo baina ya Simba na KMC ulimalizika kwa kadi nyekundu aliyoipata beki wa KMC, Andrew Vicent wakati timu hizo zilipokutana Julai 7, 2021 na Simba kushinda 2-0.
KMC ikiwa imefunga mabao matano na kuruhusu 21 katika mechi 14, inaonekana benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha mkuu, Baresi, lina kazi ya kufanya kuboresha maeneo hayo.
Wapinzani wao Simba, katika mechi saba, wamefunga mabao 14 na kuruhusu manne hivyo Kocha, Steve Barker na wasaidizi wake kwa kiasi fulani wameifanya kazi nzuri kuzipa makali safu zao za ulinzi na ushambuliaji.
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Morice Abraham, akijaribu kumtoka mchezaji wa Mashujaa katika mechi ya Ligi Kuu iliyomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa 2-0 Januari 29, 2026. Picha na Simba
Kocha wa Simba, Steve Barker amesema wanahitaji kupata matokeo mazuri katika mchezo huo:
“Maandalizi yamekwenda vizuri hadi sasa, tunahitaji kucheza mechi hiyo vizuri ikiwemo kutawala mchezo na kupata ushindi kama ambavyo malengo yetu yalivyo,” amesema Barker.
Naye kocha wa KMC, Mohamed Abdallah amesema wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao utapigwa kwenye dimba lao la nyumbani:
“Tumeamka salama na tupo tayari kwa ajili ya mchezo, kwani tutakuwa na mchezo na Simba katika dimba letu la nyumbani, tumejipanga vizuri na kujiandaa vyema, tunafahamu tunakwenda kucheza dhidi ya timu kubwa.
“Mchezo utakuwa na ushindani wa kiufundi zaidi, vijana lazima wawajibike kupambania timu, tayari wameshasikiliza maelezo na imebaki kesho kwenda kuwajibika ndani ya dakika 90,” amesema Baresi.