Uwekaji wa kumbukumbu, ziwe mbaya au nzuri, umekuwa ukipata umuhimu mkubwa tangu dahari na enzi na kuwa sehemu muhimu ya maisha ya binadamu.

Kumbukumbu ndizo zinazoakisi safari ya watu, taifa au mtu binafsi zikionesha tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.

Umuhimu huu ndio uliosababisha kuwepo kwa kile kinachoitwa historia. Neno historia limetoholewa kutoka maneno mawili ya lugha ya Kiingereza His story, yaani hadithi yake.

Maneno hayo yaliunganishwa na hatimaye kubuniwa neno historia, likiwa na maana ya kusimulia na kuhifadhi matukio yaliyopita kwa ajili ya rejea ya sasa na baadaye.

Kutokana na umuhimu wa kuwa na maelezo ya matukio, kila familia, jamii na nchi kwa ujumla huwa na utaratibu wa kuweka na kuhifadhi kumbukumbu.

Leo hii zipo kumbukumbu zilizohifadhiwa za matukio ya zaidi ya karne tano au zaidi, jambo linalothibitisha dhamira ya binadamu kuhifadhi historia yake.

Kwa mfano, nchini Misri kumekuwepo utaratibu wa kuhifadhi kumbukumbu hata za mwili wa mfalme Tutankhamun (Mfalme Tut), ambaye umaarufu wake mkubwa unatokana na nafasi yake kama Farao.

Hili linaonesha namna taifa hilo linavyothamini historia yake, bila kujali kama ni ya mafanikio au changamoto.

Hata Zanzibar ina kumbukumbu za wafalme waliotawala, nyaraka zao pamoja na kumbukumbu za chaguzi zilizofanyika kabla ya Mapinduzi, ili watu waweze kuelewa kilichotokea katika nyakati mbalimbali za historia ya nchi hiyo. Huu ni ushahidi wa wazi wa kutambua umuhimu wa kumbukumbu katika kujenga uelewa wa kitaifa.

Kwa kutambua umuhimu wa kuwepo kwa kumbukumbu, Zanzibar ilianzisha Jumba la Makumbusho lijulikanalo kama Beit el-Amaan mwaka 1925, lililopo Mnazimoja mjini Unguja. Jengo hilo lilijengwa mahsusi kuwa kumbukumbu ya watu waliopoteza maisha yao katika Vita Kuu ya Dunia ilivyoanza mwaka 1914 na kumalizika mwaka 1918.

Hata hivyo, jumba hilo pia limekusanya historia ya mambo mengi ya Zanzibar, yakiwamo maisha ya wafalme, nyaraka mbalimbali pamoja na vitu tofauti vya zamani vinavyotoa taswira ya maisha ya nyakati zilizopita.

Baadaye, mwaka 1954 ilianzishwa Ofisi ya Nyaraka iliyopo Kiminani, mjini Unguja, kwa lengo la kuhifadhi nyaraka muhimu za serikali na taifa kwa ujumla.

Hadi leo bado zipo kumbukumbu za mijadala ya Baraza la Kutunga Sheria lililokuwepo kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964, pamoja na kumbukumbu za Baraza la Wawakilishi tangu kuanza kwake mwaka 1980.

Swali linalojitokeza ni kwa nini kumbukumbu hizi hazijaharibiwa? Jibu ni rahisi: ni kwa sababu zinathaminiwa kama sehemu ya historia ya taifa.

Kwa mshangao wa wengi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilitangaza uamuzi wake wa kuchoma moto kumbukumbu za uchaguzi wa mwishoni mwa Oktoba mwaka jana.

Tangazo hilo lilikuja wakati chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kilikuwa kimeamua kufuata mkondo wa kisheria kwa kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume hiyo.

ACT-Wazalendo inadai kuwa matokeo yaliyotangazwa hayakuwa halali na si yale yaliyorekodiwa katika vituo vya kupigia kura, huku ikisisitiza kuwa wao wanazo takwimu halisi za matokeo.

Kwa mantiki hiyo, nyaraka zilizokuwepo ZEC zingesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ithibati ya ukweli au uwongo wa madai yaliyotolewa kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Zanzibar ilitoa tamko la kuzuia nyaraka hizo kuchomwa moto, na kinachosubiriwa sasa ni kuona nini kitafuata kuhusu madai hayo na mwenendo wa uchaguzi uliopita.

Hatua hiyo ya mahakama inaonesha uzito wa suala la kumbukumbu katika mchakato wa haki na uwazi.

Kwa mtazamo wangu, ZEC mbali na kueleza kuwepo kwa nia njema ya kuchoma nyaraka hizo, ingekuwa vyema zaidi kueleza wazi nia hiyo njema ni ipi hasa na ubaya gani ungekuwepo endapo nyaraka hizo zingebaki kwa muda mrefu au kuwa sehemu ya kumbukumbu za uchaguzi za Zanzibar.

Kwa bahati mbaya, ZEC ilipotangaza uamuzi huo, waandishi wa habari wachache walioalikwa mahsusi kusikiliza tangazo la kuchoma nyaraka hizo hawakudadisi wala kuomba ufafanuzi wa kina kuhusu uamuzi huo uliodaiwa kuwa na nia njema na uko kwa mujibu wa sheria.

Hali hiyo ilizua maswali kuhusu uhuru na wajibu wa vyombo vya habari katika kulinda maslahi ya umma.

ZEC ilionekana kama kuwatenga waandishi wa habari ambao wangeweza kuhoji mantiki ya uamuzi huo au kuuliza ni kwa nini kulikuwa na ulazima wa kuharakisha kuchoma nyaraka hizo badala ya kuzihifadhi kama kumbukumbu za taifa.

Kwa sasa, ZEC bado inapaswa kutoa ufafanuzi wa kina na wa wazi kwa umma, badala ya kukwepa maswali kuhusu kilichosababisha uamuzi huo na faida gani ilitarajiwa kupatikana endapo nyaraka hizo zingechomwa moto kwa haraka. Ni vyema kutambua kuwa si kwa ZEC pekee, bali kwa kila taasisi ya serikali, umma na hata binafsi, kuelewa kwamba uwekaji wa kumbukumbu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya nchi.

Watu hujipanga vyema kwa safari ya wanakokwenda endapo wataelewa walikotoka wao na wazee wao, pamoja na mahali walipofikia sasa.

Si haki kutumia kauli ya ‘nia njema’ kuhalalisha jambo lolote, kwani mara nyingine nia njema ya mdomoni haiwakilishi nia iliyopo moyoni.

Utawala bora unajengwa juu ya uwazi, uwajibikaji na uhifadhi wa kumbukumbu, iwe ni ya maandishi au sauti, hivyo ni vielelezo halisi vya kuthibitisha matukio yaliyotokea.

Kutegemea simulizi pekee ni hatari, kwa kuwa mara nyingi simulizi huongezewa chumvi, sukari au hata asali. Ni muhimu kujenga utamaduni wa uwazi na kuhifadhi kumbukumbu zitakazotuonesha ukweli wa kila jambo lililotokea Zanzibar. Historia ina umuhimu wa kipekee kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *