
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kwamba utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump unaonyesha uadui dhidi ya Umoja wa Ulaya na unataka kuuvunja.
Macron ameviambia vyombo vya habari kwamba: “Ulaya sasa inajishughulisha na utawala wa Trump ambao una uadui wa waziwazi dhidi ya Ulaya na unaonyesha dharau kwa Umoja wa Ulaya.”
Macron ameongeza kwamba “Umoja wa Ulaya haupaswi kudanganywa na hisia potofu ya usalama kwamba mvutano na Marekani kuhusu Greenland, teknolojia na biashara umekwisha.”
Kauli hii ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa inaendana na msimamo jumla wa Ulaya kuhusu Marekani, kwani ripoti iliyotolewa na Mkutano wa Usalama wa Munich imethibitisha kwamba Ulaya imetambua, kwa uchungu, haja ya kuwa na uthubutu zaidi na kujitegemea kijeshi badala ya kuwa tegemezi kwa utawala wa Marekani, ambao imeutaja kuwa ni “wa kimabavu,” ikieleza kwamba Marekani “haishikamani tena na viwango na maadili ya kidemokrasia ya kiliberali.”
Matamshi ya Macron kuhusu kile alichosema ni uadui wa Marekani dhidi ya Ulaya, yanakuja katuka anga inayotawaliwa na mvutano kati ya Wazungu wa Ulaya na utawala wa Marekani kuhusu jinsi Marekani inavyoshughulikia masuala mbalimbali, kama vile hamu yake ya wazi ya kunyakua Greenland, ushuru, Ukraine, na kadhalika.