DAR ES SALAAM; Mjasiriamali wa Kitanzania anayeishi diaspora, Chris Lukosi, ametangaza mpango wa uwekezaji mkubwa wa makazi na biashara unaojulikana kama Lukosi Village, akisema mradi huo unalenga kujenga mfumo wa kiuchumi wa muda mrefu unaounganisha minada, makazi ya muda na shughuli za uingizaji bidhaa.

Mradi huo, unaotarajiwa kugharimu mabilioni ya shilingi, utajumuisha ujenzi wa apartments za studio, one-bedroom na two-bedroom, pamoja na nyumba chache za hadhi ya juu. Kwa mujibu wa Lukosi, lengo si kuuza mali bali kuunda urithi wa kudumu wa kifamilia na kibiashara.

“Sijengi kwa ajili ya kuuza. Natengeneza empire itakayobaki kwa vizazi,” alisema Lukosi katika mahojiano maalum. “Nilipoteza nyumba yangu ya kwanza nikiwa bado kijana kwa sababu ya mikopo. Nilijifunza kwamba mali za msingi hazipaswi kuuzwa kwa pupa.”

Lukosi, anayefanya biashara ya kuingiza bidhaa kutoka Ulaya, amesema ana mpango wa kuleta zaidi ya makontena 100 ndani ya mwaka mmoja ili kupanua mzunguko wa biashara. Anasema miundombinu ya Lukosi Village itahakikisha wafanyabiashara wanaoshiriki minada wanapata malazi ya karibu na eneo la biashara, huku mali hizo zikitumika pia kama Airbnb wakati wa mapumziko ya minada.

“Tunataka wafanyabiashara wakifika hapa wapate kila kitu ndani ya eneo moja — makazi, usafiri na biashara,” alisema. “Huu ni mfumo wa kiuchumi, sio jengo tu.”

Meneja wa Huduma za Kidigitali wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Sylivestre Domasa (kushoto) akizungumza na Chris Lukosi wakati alipotembelea eneo lake la mnada Tegeta, Dar es Salaam hivi karibuni kufanya naye mahojiano.

Mbali na makazi, mradi huo utahusisha maandalizi ya bidhaa kabla ya minada, ikiwa ni pamoja na upimaji na upangaji wa vifaa vya kielektroniki kama televisheni, kompyuta na vifaa vingine vinavyoagizwa kutoka nje. Lukosi anasema lengo ni kuongeza ufanisi na uwazi katika mauzo.

Wachambuzi wa uchumi wanasema miradi inayochanganya makazi na biashara inaweza kuchochea ukuaji wa maeneo ya pembezoni mwa jiji kwa kuongeza ajira, mapato ya kodi na huduma za kijamii.

Lukosi anasema mradi wake pia unalenga kujenga utajiri wa vizazi. “Natengeneza generational wealth. Sitaki watoto wangu waanze upya pale nilipoanza,” alisema.

Chris Lukosi

Aliongeza kuwa anaona mchango wake katika kulipa kodi na kuajiri vijana kama sehemu ya uzalendo wa kiuchumi. “Ninajivunia kuchangia pato la taifa. Kila kontena linaloingia linaongeza ajira na mapato,” alisema.

Mradi huo unatarajiwa kuanza kwa awamu, huku ujenzi wa apartments ukiwa hatua ya kwanza. Lukosi anasema dhamira yake ni kuhakikisha kuwa eneo hilo linakuwa kitovu cha minada na biashara ya kimataifa ndani ya miaka michache ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *