SERIKALI juzi imezindua Mpango wa ushirikiano baina ya waajiri, vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na taasisi za elimu ya juu, ambao imesema ni wa lazima ili stadi zinazozalishwa ziwiane na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Imeeleza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inabainisha wazi kuwa ushirikiano kati ya vyuo na sekta ya uzalishaji na waajiri siyo hiari, bali ni wajibu wa kimfumo ili kuhakikisha stadi zinazozalishwa zinawiana na mahitaji halisi ya soko la ajira na uchocheaji wa ukuaji wa uchumi.
Katika kutekeleza agizo la kuwepo kwa mpango huo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeeleza kuwa imeanzisha kamati 33 za ushauri wa kitasnia, lakini pia imesaini mikataba ya ushirikiano ikiwamo 50 ya Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na mikataba zaidi ya 250 kati ya taasisi za elimu ya juu na viwanda pamoja na mikataba 76 ya vyuo vya ufundi na viwanda.
Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, tafiti zinaonesha bado kuna pengo kati ya ujuzi unaotolewa na taasisi za elimu na ujuzi unaohitajika katika sekta ya viwanda na biashara.
Wizara hiyo imebainisha kuwa waajiri wengi wamekuwa wakihitaji wahitimu wenye ujuzi wa vitendo, ubunifu na utatuzi wa changamoto, uelewa wa teknolojia za kisasa za uzalishaji na maadili ya kazi na ushindani wa kimataifa.
Ndiyo maana mpango huu ambao ni utekelezaji wa ahadi ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha pili, umekuja katika wakati mwafaka na bila shaka utakuwa mwarobaini wa matatizo hayo.
Kwa muda mrefu, kumekuwa na kilio cha waajiri kwamba vijana wanaohitimu elimu ya vyuo vya ufundi na vyuo vikuu hawana ujuzi na ubunifu na wengi wao wamekuwa watu wa nadharia zaidi kuliko vitendo, hivyo kutokidhi mahitaji ya soko la ajira ambalo limekuwa na ushindani mkubwa.
Hivyo ushirikiano huo unakwenda kuleta suluhisho kubwa katika changamoto hii ya wahitimu kwani licha ya kuwapo kwa mitaala itakayoandaliwa kuendana na mahitaji halisi ya sekta za vipaumbele, na wahitimu watamaliza masomo yao wakiwa wamepata ujuzi kwa kwenda kwenye viwanda kupata mafunzo kwa vitendo yatakayowezesha kuajiriwa au kujiajiri wanapomaliza masomo yao.
Tunaamini wanafunzi watakuwa tayari kuwa chachu ya mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo kwani wao ndio sehemu ya ubunifu ulioletwa na serikali na wana sehemu kubwa ya kushiriki mpango huu wenye tija kubwa katika kukabiliana na soko la ajira lenye kuhitaji wenye ujuzi na ubunifu.
