DAR ES SALAAM. Mjasiriamali Chris Lukosi anasema safari yake ya maisha imejengwa juu ya kanuni moja: kutokata tamaa. Akikumbuka kupoteza nyumba yake ya kwanza kutokana na changamoto za kifedha, Lukosi anasema tukio hilo lilimfundisha somo la uthabiti na maamuzi ya muda mrefu.
“Failure is not an option,” alisema. “Ukidondoka, inuka na songa mbele.”
Kwa mujibu wa Lukosi, kushindwa ni sehemu ya safari lakini hakupaswi kuwa chaguo la kudumu. Anasema vijana wengi hukata tamaa wanapokumbana na changamoto za awali za biashara au ajira.

“Usigeuke kuangalia wanaokubeza,” alisema. “Ukitumia muda wako kupambana na wakosoaji, unapoteza muda wa kusonga mbele.”
Lukosi anasema uzoefu wake ulimfundisha umuhimu wa nidhamu ya kifedha na uwekezaji wa muda mrefu. Badala ya kuuza mali mara tu inapopanda thamani, anasisitiza kujenga urithi wa kudumu.
Wataalamu wa saikolojia ya mafanikio wanasema mtazamo wa kuona kushindwa kama fursa ya kujifunza huongeza uwezo wa mtu kustahimili shinikizo na kuendelea kupambana.

Lukosi anasema ujumbe wake kwa vijana ni rahisi: kuwa na ndoto kubwa lakini pia kuwa tayari kuvumilia maumivu ya safari.
“Never say never,” alisema. “Hakuna njia ya kurudi nyuma.”-