Katika taarifa ya pamoja, iliyotolewa mjini New York Marekani wadau hao  watano wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa ghasia na kuonya kuwa matumizi ya mbinu za kivita zenye uharibifu mkubwa zaidi yanaendelea kuwaletea madhara makubwa raia wa Sudan.

“Quintet inataka kusitishwa mara moja kwa ongezeko lolote la shughuli za kijeshi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbinu za kivita zenye uharibifu mkubwa zaidi, ambazo zinaleta madhara makubwa kwa raia,” imesema taarifa hiyo.

Maelfu bado wamenaswa katika miji ya Kordofan, Darfur na El Fasher, ambako vita vinaendelea kupamba moto.

© IOM/Philippa Lowe

Maelfu bado wamenaswa katika miji ya Kordofan, Darfur na El Fasher, ambako vita vinaendelea kupamba moto.

Hofu kubwa Kordofan na Blue Nile

Quintet imeeleza hofu yake kuhusu hali inayozorota kwa kasi katika maeneo ya Kordofan na Jimbo la Blue Nile, ikitaja ripoti za mashambulizi mabaya ya ndege zisizo na rubani au drones, kuzingirwa kwa vituo vya makazi ya watu, na mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya kiraia.

Hospitali, shule na mali za misaada ya kibinadamu zimeripotiwa kushambuliwa, huku misafara ya misaada na njia muhimu za usambazaji zikikabiliwa na vitisho vikubwa. 

Watu wengi wamelazimika kuyakimbia makazi yao huku upatikanaji wa misaada ya kibinadamu ukiendelea kuzuiwa.

“Maendeleo haya yanasisitiza umuhimu wa hatua za haraka ili kuzuia ukatili zaidi,” Quintet imeonya.

Kundi hilo pia limerejea matukio ya kutisha yaliyoshuhudiwa El Fasher, likikumbusha kuwa onyo la awali halikuzingatiwa na kusababisha “madhara makubwa kwa raia.”

“Quintet inasisitiza kwamba raia hawapaswi tena kubeba gharama ya mapigano yanayoendelea,” imesema taarifa hiyo.

Sheria za kimataifa ziheshimiwe

Quintet imesisitiza kuwa ulinzi wa raia, majengo ya kiraia na miundombinu muhimu ya kitaifa ni wajibu wa msingi chini ya sheria za kimataifa, na kwamba sheria za kimataifa za kibinadamu zinawahusu wote wanaohusika katika mapigano.

“Raia na miundombinu ya kiraia lazima ilindwe, sheria za kimataifa za kibinadamu lazima ziheshimiwe, na upatikanaji salama, wa haraka na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu katika maeneo yote yenye uhitaji lazima uhakikishwe,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imetoa onyo la wazi kuhusu uwajibikaji, “Ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu haupaswi kupuuzwa. Wahusika lazima wawajibishwe.”

Mtoto wa Sudan katika KAMBI ya DALI, TAWILA - Darfur. Familia yake ilikimbia El Fasher, ambapo njaa iliyokuwa ikiendelea ilithibitishwa mnamo Oktoba 2025

Mtoto wa Sudan katika KAMBI ya DALI, TAWILA – Darfur. Familia yake ilikimbia El Fasher, ambapo njaa iliyokuwa ikiendelea ilithibitishwa mnamo Oktoba 2025

Wito wa usitishaji mapigano kabla ya Ramadhani

Kadri mwezi mtukufu wa Ramadhani unavyokaribia, Quintet imewataka wahusika wote kutumia fursa ya juhudi zinazoendelea za kufanikisha usitishaji mapigano kwa minajili ya kibinadamu, hatua ambayo inaweza kuwa msingi wa kusitisha mapigano kwa upana zaidi.

Mashirika hayo matano yamehimiza juhudi za pamoja na zenye uratibu, hasa kutoka kwa wale wenye ushawishi mkubwa, ili kupunguza kasi ya mapigano na kukomesha mtiririko wa silaha, wapiganaji na aina nyingine za msaada unaochochea ghasia na kuchangia kugawanyika kwa Sudan.

“Kwa dhamira ya umoja, Quintet inasisitiza haja ya juhudi za pamoja na zenye ufanisi kupunguza kasi ya mapigano, kurejesha mazingira yanayowezesha ulinzi wa raia, na kusitisha mtiririko wa silaha,” imesema taarifa hiyo.

Imeongeza kuwa usitishaji wowote wa mapigano lazima ufuate sheria za kimataifa, sheria za kimataifa za kibinadamu, ahadi zilizopo na maazimio husika ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwemo Azimio namba 2736 la tarehe 13 Juni 2024.

Msaada kwa mamlaka na mpito wa kisiasa Sudan

Huku ikionya kuwa kuendelea kwa ongezeko la mapigano kunaweza kudhoofisha zaidi ulinzi wa raia na miundombinu ya taifa, Quintet imethibitisha tena dhamira yake ya kuheshimu mamlaka, umoja, uhuru na uadilifu wa mipaka ya Sudan.

Kwa mtazamo wa mbele, kundi hilo limeahidi kuendelea kuwezesha mazungumzo jumuishi yanayoongozwa na Wasudan wenyewe, kwa lengo la kumaliza vita na kuweka msingi wa mpito wa kisiasa wa amani.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa “Quintet inasalia kuwa imejizatiti kuwezesha mazungumzo jumuishi yanayoongozwa na Wasudan wenyewe yenye lengo la kumaliza vita”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *