Rais wa Vladimir Putin wa Russia amefanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambapo pande hizo mbili zimejadili kuhusu suluhu inyoweza kufikiwa nchini Ukraine.

Ikulu ya Russia, Kremlin, imeeleza katika taarifa yake kuwa Rais wa Afrika Kusini amesema anaunga mkono juhudi za kidiplomasia za kutatua mgogoro wa Ukraine. 

Taarifa ya Kremlin imeeleza kuwa: Katika mazungumzo yao ya simu Marais wa Russia na Afrika Kusini wamejadili hali ya mambo nchini Ukraine na kwamba Rais Cyril Ramaphosa amesema anaunga mkono juhudi za Russia zenye lengo la kuupatia ufumbuzi mzozo wa Ukraine kwa njia za kidiplomasia na kisiasa. 

Marais hao wawili pia wametilia mkazo umuhimu wa kuendelea kuwasiliana Russia na Afrika Kusini ndani ya fremu ya kundi la G20 na BRICS. Mbali na kadhia ya Ukraine, Putin na Ramaphosa pia  wamejadili suala la kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya pande mbili.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zilizojitolea kufanya upatanishi katika  mzozo wa kijeshi kati ya Russia na Ukraine, ambao unakaribia kuingia mwaka wake wa tano.

Jumapili iliyopita Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha alisema kuwa viongozi wa Russia na wa nchi yake wanapasa kukutana ana kwa ana ili kuharakisha makubaliano kuhusu masuala nyeti yanayohusu mazungumzo ya amani.

Masuala hayo yanayotajwa kukwamisha makubaliano ni pamoja na mzozo wa ardhi. Russia inasisitiza kuwa Ukraine lazima iachie asilimia 20 ya eneo lililosalia la mashariki mwa Donetsk ambalo imeshindwa kulidhibiti katika kipindi chote cha vita, jambo ambalo Ukraine inalipinga vikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *