London, England. Tottenham Hotspur imemtimua meneja wake, Thomas Frank, miezi minane tu baada ya kumteua kushika wadhifa huo.

Menaja huyo raia wa Denmark amekuwa katika presha kubwa katika wiki za karibuni kufuatia mfululizo wa matokeo mabaya yaliyoishuhudia Spurs ikishuka hadi nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL), huku kipigo cha nyumbani cha mabao 2-1 kutoka kwa Newcastle United Jumanne kikitajwa kuwa pigo la mwisho kwa mabosi wa klabu hiyo.

Dalili za kuondoka kwa Frank aliyewahi kuinoa Brentford zilianza kuonekana miezi kadhaa iliyopita, na sasa kipindi chake kibaya kimefikia tamati.

Frank ameshinda mechi saba pekee kati ya 26 za ligi alizoziongoza, akipoteza 11, hali iliyoiacha timu yake ikiwa na tofauti ya pointi tano tu kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja.

Aliyekuwa kocha wa Tottenham, Thomas Frank wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari baada ya mechi dhidi ya Newcastle kumalizika  kwa kipigo cha 2-1 Februari 10, 2026. Picha na Mtandao

Katika taarifa ya klabu iliyotolewa Jumatano asubuhi kuthibitisha uamuzi huo, imeeleza: “Klabu imeamua kufanya mabadiliko katika nafasi ya Kocha Mkuu wa timu ya wanaume na Thomas Frank ataondoka leo.

“Thomas aliteuliwa Juni 2025, na tumekuwa na dhamira ya kumpa muda na sapoti inayohitajika kujenga mustakabali wa klabu kwa pamoja. Hata hivyo, matokeo na viwango vya uchezaji vimeifanya bodi ihitimishe kuwa mabadiliko katika hatua hii ya msimu ni muhimu.

“Katika kipindi chote alichokuwa hapa, Thomas ameonesha kujitolea bila kuyumba, akitoa kila alichonacho katika juhudi za kuisukuma klabu mbele. Tungependa kumshukuru kwa mchango wake na kumtakia mafanikio mema siku zijazo.”

Beki wa Tottenham, Radu Dragusin akionekana mwenye huzuni baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle, jana Februari 11, 2026. Picha na Mtandao

Chini ya Frank, Spurs pia walitolewa kwenye Kombe la FA katika raundi ya tatu baada ya kufungwa na Aston Villa, na katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Carabao waliondolewa na Newcastle, ingawa waliweza kumaliza nafasi ya nne katika hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, timu hiyo imeshindwa kuhamisha mafanikio yao ya Ulaya hadi kwenye Ligi Kuu England, mashindano ambayo Spurs hawajashinda mechi tangu Desemba 28, wakicheza michezo minane bila ushindi.

Katika mechi sita zilizopita za ligi, wamekusanya pointi mbili pekee, huku Frank na wachezaji wake wakizomewa vikali wakati na baada ya kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Newcastle.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 pia alikumbwa tena na nyimbo za mashabiki wake wakisema “atafutwa kazi asubuhi”, ishara ya wazi ya kukosa imani kwa uongozi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *