
Donald Trump anampokea Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo Jumatano Februari 11, ambaye anatataka kumshawishi atoe shinikizo la juu zaidi kwa Iran.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kabla ya mkutano huu, wa saba tangu arudi madarakani mwaka mmoja uliopita, rais wa Marekani ametuma mfululizo wa ishara zeye utata, kati ya matumaini ya makubaliano na vitisho vya kijeshi dhidi ya Tehran.
Kilicho hatarini kwa Netanyahu
“Mazungumzo yoyote (kati ya Iran na Marekani) lazima yajumuishe ukomo wa makombora ya balestiki na kusitishwa kwa usaidizi kwa mhimili wa Iran,” akimaanisha makundi yenye silaha yenye uhusiano na Tehran katika eneo hilo, amebainisha Benjamin Netanyahu, ambaye anaichukulia Jamhuri ya Kiislamu kama tishio la kuwepo kwa nchi yake.
Suala la kombora ni mstari mwekundu kwa Israel, ambayo inapatikana takriban kilomita 2,000 kutoka Iran.
Benjamin Netanyahu amekuwa akisema kwa miaka mingi kwamba hatua za kijeshi ndiyo njia pekee ya kutatua suala la nyuklia la Iran. Marekani ilishmbulia maeneo ya nyuklia ya Iran wakati wa vita vya siku 12 vilivyozinduliwa na Israel mwezi Juni.
Waziri Mkuu wa Israel, anayekabiliwa na tishio la uchaguzi wa mapema, anaweza pia kuwa na matumaini ya kupata uungaji mkono wa kisiasa kwa kujitokeza pamoja na Donald Trump, ambaye ni maarufu sana nchini Israel.
Kutoka Australia, ambapo kwa sasa yuko ziarani, Rais wa Israel Isaac Herzog amesema anatumai mkutano kati ya viongozi hao wawili utasaidia kupambana na kile anachokiita Iran, “nchi ya maovu.”
Huko Washington, Bw. Netanyahu alikutana siku ya Jumanne jioni na mjumbe wa rais wa Marekani, Steve Witkoff, na mkwewe Donald Trump, Jared Kushner. “Walijadili masuala ya kikanda na kupitia duru ya kwanza ya mazungumzo waliyofanya na Iran Ijumaa ya wiki iliyopita,” kulingana na taarifa kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israel.
Msimamo wa Trump uko je?
“Ningependa kufanya makubaliano. Lazima yawe makubaliano mazuri, hakuna silaha za nyuklia, hakuna makombora, hapana hiki, hapana kile,” rais wa Marekani alisema siku ya Jumanne kwenye Fox Business.
Alitangaza kwamba Wairan watakuwa “wapumbavu” wakikataa, huku akionekana kuhoji uaminifu wa utawala wa Iran, ambao alisema hawakuwa “wakweli na waaminifu” hapo awali.
Donald Trump pia aliambia tovuti ya Axios kwamba “anafikiria” kuongeza meli ya pili kubwa kwa kikosi cha majini cha Marekani kilichotumwa katika eneo hilo.
Katika tukio la mazungumzo, “Trump lazima aweze kuonyesha kwamba makubaliano hayo, ikiwa yapo, ni bora zaidi kuliko yale aliyoyaacha,” yaliyofikiwa huko Vienna mnamo 2015 na kushtumiwa na rais huyo kutoka chama cha Republican mnamo 2018 wakati wa muhula wake wa kwanza, kulingana na Guy Ziv, profesa msaidizi wa sera za kigeni katika Chuo Kikuu cha Marekani.
“Njia moja ya kuhakikisha hili, bila shaka, ni kujumuisha makombora,” ambayo hayakuingizwa katika makubaliano ya awali, lakini “kuna uwezekano mkubwa kwa Wairani watakubali hili,” ameiambia shirika la habari la AFP.
Mazungumzo
Baada ya mazungumzo ya awali mnamo Februari 6 huko Oman, Washington na Tehran walisema wanataka kuendelea na mazungumzo, ingawa misimamo yao inaonekana kutofautiana sana.
Iran inataka tu kujadili mpango wake wa nyuklia
Marekani pia inataka kujumuisha vikwazo kwenye uwezo wa makombora ya balestiki na kukomesha usaidizi kwa makundi yenye silaha yanayopinga Israei, kama vile waasi wa Houthi huko Yemen, kundi la wanamgambo wa Kiislamu nchini Lebanon la Hezbollah, na Hamas huko Palestina.
Siku ya Jumanne, Tehran ilitoa wito kwa Marekani kupinga “ushawishi wa uharibifu” ambao unaweza kukwamisha kuanza tena kwa mazungumzo, ikiishutumu Israel kwa kutenda “kama mhujumu.”
Mwaka wa 2024, Iran ilizindua mashambulizi mawili ya makombora dhidi ya Israel. Wakati wa vita vya siku 12 mnamo mwezi Juni 2025, Marekani ilijiunga na mshirika wake katika kushambulia maeneo matatu ya nyuklia ya Iran, ikiwa ni pamoja na Natanz.
Donald Trump anaendelea kujivunia mafanikio na nguvu ya operesheni hii, ingawa mashaka yanabaki kuhusu kiwango cha athari zake kwenye uwezo wa Iran.
Ukingo wa Magharibi
Israel imeamua kuimarisha umiliki wake katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa, ambayo inaweza kuruhusu upanuzi wa makazi katika Ukingo wa Magharibi, na kusababisha lawama kubwa za kimataifa.
Donald Trump “haungi mkono hatua ya Israel ya kunyakua Ukingo wa Magharibi,” afisa wa utawala wa Trump alibainisha siku ya Jumatatu jioni.
Hata hivyo, Marekani, mshirika mkuu wa Israel, imejiepusha na ukosoaji wowote wa wazi.