Dar es Salaam. Moja ya nyimbo zinazotamba katika msimu huu wa Valentine ni ‘Valentine si Coming’. Wimbo unaoongezwa mistari kila mwaka, ambapo 2026 tayari umefikisha verse ya sita.

Wimbo huo umeimbwa na kikundi cha muziki kutoka Nigeria kiitwacho Kabusa Oriental Choir. Kinajulikana kwa mtindo wake wa kipekee wa kuimba nyimbo maarufu katika mtindo wa kwaya za kanisani.

Februari 2020, Kabusa waliamua kufanya wimbo maalum wa Siku ya Wapendanao uitwao ‘Valentine is Coming’. Wimbo huo ukawa maarufu kimataifa huku ukisikilizwa kwenye BBC 1XTRA Radio wiki ya Valentine na kuufanya ufuatiliwe na watu wengi.

“Valentine inakuja,
Yuko wapi mpenzi wako?
Umekaa nyumbani (oh chale oh),
Uko mpweke sana.

“Abena, Abena, Abena, Abena,
Yuko wapi mpenzi wako?
Wenzako wanapata maua,
Wewe uko mpweke sana,
” inasikika mistari ya wimbo huo.

Tangu wakati huo, Kabusa wamekuwa wakitengeneza mistari mipya (verses) ya wimbo huo kila mwaka. Wakibadilisha hadithi kidogo na kuongeza ucheshi na kuufanya wimbo uwe wa kuvutia kila mwaka ambapo 2026 wimbo huo upo verse ya 6.

Kabusa Oriental Choir ni nani?

Kabusa Oriental Choir ni kikundi cha choir kutoka Nigeria kinachojulikana kwa kuingiza ucheshi katika nyimbo maarufu zinazotolewa na mastaa wakubwa. Huku wakiimbia kama kwaya ya kanisani.

Kikundi hiki kilianzishwa Machi 11, 2019 na Austin Chinemezu Nwamara, ambaye ni Mkurugenzi.  Baada ya kuchapisha wimbo wao wa kwanza ambao ulikuwa mchanganyiko wa wimbo wa Yeba na Baba,ulipata umaarufu zaidi katika mitandao ya kijamii.

Wazo la kuanzisha mtindo huo wa uimbaji ulitokana na Mkurugenzi Nwamara wakati alipokuwa kwenye usafiri wa Uber akirudi nyumbani akitoka kwenye ofisi yake ya sheria huko Abuja, Nigeria. Alianza kuimba wimbo wa ‘Baba’ wa Kizz Daniel kama kwaya ya kanisa Katoliki jambo lililofanya mwenzake na dereva wa Uber wacheke. Ndipo aligundua kuwa wimbo huo ungeweza kuwa maarufu.

Baada ya kupita wiki alifanikiwa kwenda studio na kurekodi kisha alichapisha katika mitandao ya kijamii. Baada ya hapo walianza kupata umaarufu na kuanza kuingiza verse katika nyimbo nyingine, zikiwemo Call Me Back na Sirens of Lesbos Featuring Sadboi, Nem Tenta na Sued Nunes, Falling Feels Like Flying na Anotr, My G ya Kizz Daniel, Rise Up na DJ Neptune ft. Laycon, Ladipoe, Waje na nyinginezo.

Aidha kwenye mahojiano waliyowahi kufanya na Zupa Media wamefichua namna wanavyopata wasanii katika kwaya yao. Wakieleza kuwa huwa wanafanya usaili.

“Ndiyo, tunafanya auditions mara kwa mara. Pia kuna watu wanaotutumia ujumbe wakitaka kujiunga. Tunawafanyia usaili, na wakifaulu wanaingia rasmi. Kwaya ni kubwa sana kwa sasa tuna karibu wanachama zaidi ya 60,”

Kuhusu kuingia kwenye muziki wa Afrobeat

“Tayari tupo ndani ya Afrobeat iko kwenye damu yetu. Tunaweza kuifanya hata usingizini. Lakini pia tunafanya aina nyingine za muziki kama trap, drill, ballad. 

“Miaka ijayo tunapanga kutoa album itakayokuwa na mitindo tofauti kutakuwa na rock (hata choir rock!), hip-hop, na Afrobeat katika mtazamo mwingine mpya. Tunaingia kwenye kila aina ya muziki,” wameeleza

Kikundi hicho kilipata mafanikio mbalimbali ikiwemo kupata tuzo ya Best in Music Comedy katika toleo la pili la Humour Award mwaka 2023. Pia kilifanikiwa kuongoza The African Beats Festival huko Dworek Pod Wiecha, Poland. Tukio ambalo lilifanyika Agosti 9,2024. 

Mpaka kufikia sasa kikundi hicho kimekuwa kikifuatiliwa zaidi, ambapo kimekuwa kikipata zaidi ya wafuatiliaji 800,000 kila mwezi kwenye Spotify. Aidha tayari wametembelea mataifa mbalimbali kwa ajili ya kupiga show ikiwemo Germany, Poland, France, Turki na Swezland.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *