Dar es Salaam. Fursa za ajira, mafunzo ya ujuzi na mchango katika pato la Taifa zimeendelea kuwa mkombozi kwa wananchi, kufuatia mpango wa Taasisi ya Epvate and Fortune International kuongeza ajira kutoka Watanzania 500 wa sasa hadi kufikia 1,000, hususan kwa vijana.
Hatua hiyo inatajwa kuwa sehemu ya juhudi za taasisi hiyo katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, kuongeza kipato kwa kaya na kuchangia kwa vitendo ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mbali na ajira, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya ujuzi na huduma za ushauri wa kitaaluma, hatua inayowawezesha vijana kujiajiri, kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujenga uwezo wa kujitegemea.
Akizungumza leo Jumatano Februari 11, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi rasmi wa Bodi ya Ushauri ya taasisi hiyo uliofanyika katika makao makuu yake, Mwenyekiti wa Epvate and Fortune International, Dk Peter Mapigano, amesema mpango wa kuongeza ajira ni sehemu ya mkakati wa kupanua shughuli za taasisi hiyo ndani na nje ya nchi.
Dk Mapigano amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2017 kwa lengo la kusaidia wananchi katika nyanja za ajira, uchumi na ushauri wa maendeleo, huku ikilenga kuwapa vijana nafasi za ajira na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Tumeajiri zaidi ya Watanzania 500 hadi sasa, na mpango wetu ni kuongeza idadi hiyo hadi kufikia ajira 1,000, sambamba na kuendelea kutoa mafunzo ya ujuzi yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi,” amesema Dk Mapigano.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo pia inachangia pato la Taifa kwa kulipa kodi ya zaidi ya Sh milioni 300 kila mwezi, hatua inayosaidia Serikali katika kugharamia huduma za kijamii na miradi ya maendeleo.
“Shughuli zetu hazipo hapa nchini pekee, bali pia katika mataifa ya nje, jambo lililotuwezesha kuajiri Watanzania wengi katika kazi za ushauri na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali,” ameongeza.
Kwa upande wake, mgeni rasmi wa hafla hiyo, Profesa Omari Mbura kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ameipongeza taasisi hiyo kwa mchango wake katika kuongeza ajira, kujenga ujuzi na kupunguza umasikini.
Profesa Mbura amesema taasisi binafsi zina nafasi kubwa katika maendeleo ya Taifa kwa kuwa zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja kupitia ajira, mafunzo na ulipaji wa kodi.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, akiwemo Joseph Yohana na Naomi Emmanuel, wamesema uwepo wa taasisi hiyo umeleta matumaini mapya kwa vijana wengi wanaotafuta ajira na fursa za kujikwamua kiuchumi.
“Taasis kama hizi zinatoa mwelekeo mpya kwa vijana na kuchangia kwa vitendo kuboresha maisha ya wananchi,” amesema Joseph Yohana.
Naomi Emmanuel amesema Epvate and Fortune International ni mfano wa taasisi binafsi zinazochangia maendeleo ya jamii kwa kuzingatia ajira, ujuzi na uzalendo wa kulipa kodi.