Afrika Kusini. Vaibu la wimbo wa Vulindlela ukipigwa katika kumbi mbalimbali za starehe, linahamasisha watu kunyanyuka vitini na kuanza kucheza kutokana na mdundo wake unavyovutia.

Mwanamuzi nguli, Brenda Nokuzola Fassie aliyezaliwa Novemba 3, 1964 Afrika Kusini na kufariki dunia Mei 9, 2004 akiwa na umri wa miaka 40 ndiye mtunzi na mwimbaji wa wimbo huo.

Mashairi ya wimbo huo ni zaidi ya mapenzi, nyuma yake kuna ujumbe wa harakati za ukombozi wa ubaguzi wa rangi kutoka kwa makaburu dhidi ya watu weusi.

Vulindlela ni neno la Kizulu kwa Kiswahili ni pisha njia, safisha njia na kwa Kingereza ni ‘Open the way,” “Clear the path,” or “Make way.

Wimbo huu unahusu kuwapisha bwana harusi (na bibi harusi) wakati wa sherehe ya ndoa yao. Mwaka 1997 Afrika Kusini ilikuwa ikijinasua kutoka katika mfumo wa kibaguzi, hivyo ulitumika kwa namna nyingine kama hamasa ya kujikomboa.

Baada ya kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia mwaka 1994, uliomweka madarakani Nelson Mandela, wimbo huo ukawa unatumika zaidi katika sherehe mbalimbali na mwaka 1997 ukapata umaarufu zaidi.

Fassie alitumia wimbo huo kuvunja mifumo na kupinga kulazimishwa kuishi vijijini maeneo pembezoni mwa mji, yaliyotengwa kwa ajili ya watu weusi na watawala wachache wa makaburu, jambo lililokuwa limempa heshima kubwa Afrika. Alianza kupanda ngazi za umaarufu katika vitongoji vya watu weusi miaka ya 1980, hakuchukua muda kuuteka muziki wa taifa zima kupitia redio na vyombo vya habari vilivyokuwa vimetawala kuzungumzia anachokifanya.

Ukiachana na wimbo wa Vulindlela, nyimbo zake maarufu baadhi yake zilikuwa Weekend Special, Too Late for Mama, na Black President, zilijumuisha nguvu za disko, ujumbe wa kisiasa, hisia pamoja na matumizi ya lugha za asili.

Pia kati ya albamu zake mwaka 1996 Now Is the Time, Papa razzi (199 7), Memeza (1998) na Nomakanjani (1999), zilipata mauzo ya kiwango cha platinamu mara nyingi nchini  humo na Memeza ikawa albamu iliyouzwa zaidi.

Ingawa aliacha alama kubwa Afrika, ripoti ya uchunguzi wa maiti ilibaini kuwa Fassie alikuwa ametumia dawa za kulevya aina ya cocaine kupita kiasi, jambo lililosababisha kulazwa kwenye coma akisaidiwa kupuma kwa mashine na akiwa hospitalini alitembelewa na Nelson Mandela (enzi za uhai wake), Winnie Mandela na Thabo Mbeki.

Msanii wa muziki wa kike, Sarah Michael Kitinga ‘Phina’ anayetrendi katika mitandao ya kijamii kutokana na kufanya kazi za kimuziki karibu na Eni, raia wa Nigeria, anasema yapo mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa wanamuziki waliowatangulia. “Aina ya uandishi wa nyimbo zao ambazo zinaweza zikawa na tafsri zaidi ya moja, kama hiyo unayoizungumzia ni kitu kizuri na kilipokewa vizuri kwa mashabiki kinaishi hadi sasa,” anasema.

Msanii Hip Hop Bongo, Abdullah Jamal Mnete ‘Zaiid’ anasema: “Huo ni utunzi wa sanaa, unaozungumzia vitu vingi kwa wakati mmoja, ndani ya wimbo wa Vulindlela kuna mapenzi pia harakati za ukombozi wa Afrika Kusini. Anaongeza: “Ni kama wimbo wangu wa Tafuta Bwana, una maana ya kumtafuta Mungu, wanawake kutafuta wanaume wawaoe na wanaume watafute pesa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *